Baadhi ya wafugaji wa eneo la Ngorongoro wakiwa katika maandamano ya kupinga kuhamishwa kutoka eneo hilo./Picha: TRT Afrika

Wakati sakata la uhamishaji wakazi kutoka ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro likiendelea kuvuta macho na masikio ya wengi kitaifa na kimataifa, kauli ya hivi karibuni ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) wa Tanzania, Mohamed Mchengerwa imezua mjadala mwingine.

Katika taarifa yake, Waziri huyo alitangaza hatua ya kuvifuta vijiji vyote vilivyomo ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, kama hatua ya kuendelea na mchakato wa kuwahamisha wakazi wa eneo hilo kuelekea kijiji cha Msomera, kilichopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Tanzania.

Kwa ufupi, tarafa ya Ngorongoro ambayo inakaliwa na jamii ya wafugaji wa jamii ya Kimaasai ina jumla ya vijiji 25, kata 11 na vitongoji 96.

Utekelezwaji wa hatua hiyo ni kulingana na Kifungu cha 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa nchini Tanzania.

Hatua hii inakuja kukiwa na taarifa za wapiga kura wa Ngorongoro kuhamishiwa wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Jumla ya wakazi 8000 kutoka jamii za kifugaji za Wamaasai wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro wamepelekwa kijiji cha Msomera, Tanga katika zoezi ambalo serikali ya Tanzania, inaliita la 'hiari'.

Hata hivyo, wakazi waliobaki katika eneo la Ngorongoro wameoneshwa kusikitishwa na mchakato mzima wa uhamishwaji kutoka eneo hilo, ili kupisha shughuli za kihifadhi.

Wakazi hao walionesha hisia zao wa wazi wakati wa maandamano yao ya amani ambayo kwa kiasi fulani, yalitatiza shughuli za utalii kati ya Ngorongoro na Serengeti, hivi karibuni./Picha: TRT Afrika

"Waziri hana Mamlaka ya kufuta vijiji au vitongoji na kifungu alichotumia hakimpi Mamlaka hiyo. Uamuzi huo ni batili na haramu," anaandika Boniface Mwabukusi Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), katika ukurasa wake wa X.

"Tumeliona tangazo la Waziri mwenye dhamana…nimepitia vifungu hivyo, kama Wakili na Mwanasheria, hakuna kifungu chcocte cha sheria kinachompa yeye mamlaka ya kile alichofanya” amesisitiza Mwabukusi.

Kwa mujibu wa Rais huyo wa TLS, waziri huyo amekitafsiri kwa upotofu Kifungu hicho cha 30, jambo ambalo ni kinyume na sheria.

"Waziri hana hiyo mamlaka kwa mujibu wa sheria hiyo aliyotumia, kama TLS, tutahahakisha kuwa wakazi wa Ngorongoro, hususani wa jamii ya Kimasaai hawaendelei kunyanyaswa, kupuuzwa na kuonewa ndani ya ardhi yao ya asili walioumbiwa na Mungu," ameongeza.

Mwaka 2021 serikali ya Tanzania ilikuwa iliweka mpango wa kuwahamisha takribani watu 82,000 wa jamii ya Kimaasai kutoka katika makazi yao katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Serikali ya kikoloni ya Waingereza ilianzisha NCA mwaka 1959, eneo linalotambulika kwa matumizi mseto na kuanzisha makazi ya kudumu ya watu waliokuwa wanaishi ndani na maeneo yanayozunguka bonde la Ngorongoro, wengi wao wakiwa ni wafugaji wa asili ya Kimaasai.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Msaada wa Sheria ya CiLAO, Charles Odero anaiambia TRT Afrika kuwa uamuzi wa kuvifuta vijiji hivyo ni kuwanyima haki ya kidemokrasia wanannchi wa Ngorongoro na jamii zao.

Kulingana na Odero, uamuzi wa Mchengerwa unaiondoa tarafa nzima ya Ngorongoro inayopatikana kaskazini mwa Tanzania, katika orodha ya wapiga kura katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

"Taarifa za wapiga kura wote wa Ngorongoro zote zimehamia Msomera, ikiwemo ya mbunge wao pia," anasema.

Kwa mujibu wa Odero, ili Waziri husika achukue uamuzi wa kukifuta kijiji, ni lazima kuwepo sababu za msingi za kufanya hivyo.

Sababu hizo ni pamoja na kubadilisha matumizi ya eneo husika na kadhalika.

"Kwa mfano, eneo husika linageuzwa kuwa pori la akiba, basi lazima mchakato wa kufuta kijiji uendelee," anaeleza Mkurugenzi Mtendaji huyo wa CiLAO.

Kulingana na Odero, kifungu tajwa cha 30, kinampa Waziri husika mamlaka ya kupitia upya, kuongeza na hata kutengeneza mipaka ya eneo na si vinginevyo.

"Unapofuta kijiji, maana yake unawaondoa kabisa wananchi wa eneo hilo."

Odero anasisitiza kuwa wananchi wa Ngorongoro wataendelea kuandamano na kupaza sauti zao hadi pale Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan atakapotoa tamko kuhusiana na jambo hilo ambalo limeibua mjadala mkubwa nchini humo.

TRT Afrika