Tanzania ina jumla ya vyama 18 vya kisiasa vilivyosajiliwa vya upinzani ambavyo vinakidhi kushiriki uchaguzi huo/ Picha: Wengine 

Hivi karibuni kipenga cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini Tanzania kitalia.

Tayari, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi imetangaza Novemba 27 kuwa ndio siku rasmi utakaofanyika uchaguzi huo.

Mfumo wa muundo wa serikali ya Tanzania, uko tofauti kidogo ikilinganishwa na nchi nyengine za Afrika Mashariki.

Tanzania, mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa kumchagua Rais na wabunge, kwanza hufanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao hutumika kusimika viongozi mbalimbali katika ngazi za mashinani ikiwemo, wenyeviti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji pamoja na wenyeviti wa kitongoji katika mamlaka za miji midogo.

Tundu Lissu ni kati ya viongozi wa upinzani / Picha: Reuters 

Uchaguzi huu ni muhimu katika siasa za Tanzania, na mara nyingi, hutumiwa na wanasiasa kuonyeshana mabavu lakini vile vile kujipima nguvu na hatimae kutoa taswira ya jinsi uchaguzi mkuu utakavyokuwa mwakani.

Tanzania ina jumla ya vyama 19 vya kisiasa vilivyosajiliwa ambavyo vinakidhi kushiriki uchaguzi huo.

Kimoja kati ya hivyo, kikiwa ndio chama tawala, CCM.

Hata hivyo, kuna haja ya kuangalia nafasi ya upinzani kuelekea uchaguzi huo.

Je, wamejipanga ipasavyo?

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania wanaona tangu uchaguzi mkuu uliopita, bado upinzani haujaweza kusimama wima na kujiimarisha ili kukabiliana na mazingira ya sasa.

Wenyewe wanadai, hii imesababishwa na mazingira magumu ya kufanya siasa huru yaliyochangiwa na CCM, hasa kipindi cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo, John Pombe Magufuli.

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, akiongoza Kikao cha Mashauriano cha Vyama vya Siasa kilichohuduriwa na viongozi wa vyama hivyo, na mawaziri na manaibu waziri/ Picha kutoka CCM

Lakini hata baada ya upinzani kuruhusiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mikutano ya hadhara, wadadisi wa mambo bado wanadai, upinzani umekosa mvuto hasa baada ya kukosa hoja za kuwateka wananchi.

Wadau mbalimbali wanafuatilia kwa karibu kuona ni jinsi gani uchaguzi wa mwaka huu utakavyofanyika, ikikumbukwa kwamba, uchaguzi uliopita, vyama kadhaa vilijitoa katika uchaguzi huo kwa madai mbalimbali ikiwemo kuenguliwa kwa wagombea na wasimamizi wa uchaguzi.

Kwa upande wake, CCM kupitia Katibu Mkuu wake, inaonyesha utashi wa kujenga mazingira sawa katika uchaguzi, ingawa upinzani unalalamika hapa na pale.

Hata hivyo, vyovyote itakavyokuwa, uchaguzi huu pia, utakuwa ni kipimo kwa Rais Samia cha utashi wake wa kukuza demokrasia na kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki.

TRT Afrika