Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu. Samia Suluhu Hassan, akiongoza Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kilichokutana tarehe 29 Novemba, 2023 Ikulu Jijini Dar es salaam. | Picha: CCM 

Kujiuzulu kwake kumejiri katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika jijini Dar es Salaam ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amekiri kupokea barua ya kujiuzulu kwa katibu mkuu wake, na kusema ameridhia ombi hilo.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Paul Makonda aliwaambia waandishi wa habari, “Mwenyekiti wa CCM amejulisha Halmashauri kuu ya CCM Taifa kupokea barua ya kujiuzulu ya Ndugu Daniel Chongolo na kuridhia ombi hilo.”

Hata hivyo, kikao hicho kimeteua wagombea wa nafasi za uongozi ndani ya Chama kwa ngazi ya Mkoa na Wilaya ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo na uteuzi wa nafasi nyingine.

Siku chache zilizopita zilisambaa taarifa kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, alimuandikia barua mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Samia Suluhu Hassan akiomba kujiuzulu nafasi hiyo.

Shauku kubwa ilikuwa ni kusubiri maamuzi ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama (NEC), ambayo inaendelea na vikao vyake jijini Dar es Salaam.

Kulingana na barua hiyo ya Chongolo aliyowasilisha kwa mwenyekiti wa Chama imeeleza kuwa miongoni mwa sababu za kutaka kujiuzulu kwake ni kuchafuliwa katika mitandao ya kijamii.

Haijulikani ni nani atakuwa mrithi wa Chongolo, na bila shaka hili ndilo swali kuu kwa sasa.

TRT Afrika