Chuo Kikuu cha Ankara cha nchini Uturuki kinatarajiwa kumtunuku Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan udaktari wa heshima katika uchumi, kama kutambua jitihada zake kuendeleza mageuzi ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi ambayo yameboresha ustawi wa Watanzania.
Kupitia ukurusa wake wa X, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania January Makamba amesema kuwa uamuzi huo umefikiwa na Baraza la Chuo Kikuu cha Ankara cha nchini Uturuki.
"Juhudi zake zimeinua hadhi ya Tanzania duniani na kuimarisha mahusiano yake ya kibiashara, kiuchumu na kisiasa na nchi zingine, ikiwemo Uturuki," Makamba ameandika.
Kulingana na Waziri huyo, Rais Samia anategemea kupokea shahada hiyo Aprili 18, 2024 katika Chuo Kikuu cha Ankara, katika tukio litakalohudhuriwa na uongozi mzima wa chuo hicho, mawaziri, wanadiplomasia na wasomi.
Hii inakuja wakati Rais Samia amewasili nchini Uturuki kwa ziara ya kiserikali.
Kwa mujibu wa Makamba, Rais Samia analenga kutumia ziara hiyo ya kiserikali kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji kuja kuwekeza nchini Tanzania.
"Uturuki ni chanzo muhimu cha uwekezaji na mapato ya nje. Ziara hii inalenga kuimarisha hili," amendika Makamba kupitia ukurasa wake wa X.