Wajumbe kutoka kamati za Bunge la Tanzania, inayohusika na miundombinu na Bajeti zimelishauri Shirika la Reli nchini humo (TRC) kufunga kamera za usalama (CCTV) kwa nia ya kudhibiti wahalifu wanaohujumu miundombinu ya reli hiyo ya kisasa.
Kamati hizo pia imeitaka TRC kuweka uzio kwenye reli ya SGR ili kudhibiti watu wenye nia ovu na miondombinu hiyo.
“Watu wameanza kukata nyaya za umeme, wakihujumu reli ambayo uwekezaji wake ni mkubwa, hivyo tunashauri shirika liweke uzio maalumu na kamera za CCTV,” alisema Selemani Kakoso ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.
Mbunge huyo alidai kuwa kuna Watanzania wachache, waliokosa uzalendo na kuamua kuhujumu miondombinu ya TRC.
“Miradi kama hii ni lazima iangaliwe kwa jicho la tatu na kwa uangalifu mkubwa,” alieleza.
Kulingana na Kakoso, serikali ilihairisha miradi mingine ili kutoa nafasi ya utekelezaji wa mradi wa SGR, ambayo ni reli ya kisasa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika taarifa yake kwa umma ya Novemba 6, 2024, Shirika la Reli Tanzania lilikiri juu ya uwepo wa hujuma iliyofanywa na baadhi ya watu kwenye miundombinu ya Treni za EMU, maarufu kama ‘treni mchongoko’.
Kwa mujibu wa TRC, baadhi ya watu waliohusika na hujuma hiyo wamekamatwa huku hatua stahiki dhidi yao zikichukuliwa.