Uhaba wa marubani nchini Tanzania umeilazimu nchi hiyo kuajiri wageni kwa gharama kubwa, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema.
Ili kukabiliana na pengo la wafanyakazi, shirika hilo sasa limelazimika kuanzisha mradi wa mafunzo ya urubani, Hamza Johari, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, alisema wakati wa maonyesho ya kimataifa ya biashara jijini Dar es Salaam Ijumaa.
“Kampuni zetu zinalazimika kuwatafuta marubani kutoka kampuni nyingine. Hii imesababisha kutegemea kuwaajiri marubani kutoka nje ya nchi, jambo ambalo linatugharimu sana,'' alisema Johari.
"Sasa tumezindua makundi ya wanafunzi shuleni ili kuwapa chachu ya kuchukua masomo ya sayansi na kuongeza idadi ya wataalam katika sekta ya usafiri wa anga."
TCAA inasema kuna takriban watu kumi kwa sasa wanaosomea urubani kupitia mpango unaofadhiliwa na shirika hilo.
Data za serikali ya Tanzania zinaonyesha inagharimu wastani wa dola 50,000 kutoa mafunzo kamili kwa marubani nchini humo.
Idadi kubwa ya marubani wa kigeni
Kufikia mwaka 2021, Taifa hilo la Afrika Mashariki lilikuwa na jumla ya marubani 562 waliosajiliwa, kati yao 321 (57.1%) wakiwa wageni na 241 (42.9%) raia wa Tanzania, kwa mujibu wa halmashauri ya kitaifa ya usafiri wa ngani (TGFA).
Nchi jirani ya Kenya ilikuwa na marubani 8,441 waliosajiliwa kufikia Machi 2022, rekodi za Mamlaka ya Usafiri wa Anga (KCAA) zinaonyesha.
Kuna takriban mashirika 12 ya ndege nchini Tanzania, na karibu yote yanafanya safari za ndani au za kikanda pekee.
Chini ya uongozi wa marehemu rais John Magufuli, nchi hiyo ilinunua ndege mpya 12 katika juhudi za kufufua shirika la kitaifa la ndege Air Tanzania.
Mwezi Juni, Rais Samia Hassan alizindua ndege mpya ya shirika hilo ya kusafirisha mizigo.
Shirika hilo la ndege linalomiliki ndege 12 pia limeongeza idadi ya vituo vinavyohudumu ndani na nje ya nchi hadi 26.
Safari ya maeneo mapya
Baadhi ya njia mpya ambazo Air Tanzania inataka kuruka ni London (Uingereza), Dubai (UAE), Muscat (Oman), Accra (Ghana), Lagos (Nigeria), Juba (Sudan Kusini) na Lilongwe (Malawi).
Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo Ladislaus Matindi aliiambia kamati ya Bunge Mei 2023 kuwa wastani wa wasafiri wanaotumia Air Tanzania kila mwezi umeongezeka kutoka 4,000 mwaka 2016 hadi 90,000 mwaka 2023.
Kwa sababu ya njia zilizoongezeka, kampuni imeajiri wafanyakazi zaidi, wakiwemo marubani na wahandisi. Kwa sasa Air Tanzania ina marubani 106 na wahandisi 129, kutoka 11 na 27 mtawalia mwaka 2016.
Mishahara ya juu na gharama zingine za uendeshaji zimesalia kwani ni changamoto kuu kwa faida ya shirika la ndege, Matindi alisema.