Tume hiyo itakuwa na watu 19, kulingana na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa./Picha:Wengine

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, ametangaza kuunda tume maalumu itakayochunguza chanzo cha kuporomoka kwa jengo la kibiashara katika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam Novemba 16, 2024.

Majaliwa, ambaye alikuwa akizungumza wakati wa shughuli maalumu ya kuwaaga waathirika 15 waliopoteza maisha katika tukio hilo, alisema kuwa tume hiyo ya wataalamu itaundwa na watu 19, ikiwa na jukumu la kuyapitia maghorofa yote katika eneo hilo maarufu kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

"Tume hiyo itasaidia kujua na kuishauri serikali baada ya uchunguzi wao, kwani mahitaji ya soko la Kariakoo ni makubwa sana, kwani ni eneo linalotegemewa na nchi zote za jirani," alisema Majaliwa.

Watu wapatao 16 wamepoteza maisha na wengine 86 wamejeruhiwa katika tukio hilo./Picha: Wengine

Kwa mujibu wa Majaliwa, ripoti itakayotolewa na timu hiyo itakayoongozwa na Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, ambaye ni Mkuu wa Menejimenti ya Idara ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, inalenga kutoa miongozo na kanuni sahihi za ufanyaji biashara katika eneo hilo.

"Hadidu za rejea zitaandaliwa kwa ajili ya tume hiyo, huku eneo hilo likiachwa wazi kwa shughuli za uokoaji," alieleza.

Wakati huo huo, Majaliwa ameliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta mmiliki wa jengo hilo, kwa uchunguzi zaidi wa kujua chanzo cha kuporomoka kwake na kusababisha maafa.

TRT Afrika