Serikali ya Tanzania imesema kuwa uamuzi wa kubatilisha leseni za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ulitokana na maduka hayo kukutwa na makosa mbalimbali yakiwemo ya kujihusisha na uhamishaji wa fedha nje ya nchi bila kuwa na leseni cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kulingana na Naibu Waziri wa Fedha wa Tanzania, Hamad Hassan Chande mwaka 2016, Benki Kuu ya Tanzania ilifanya ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na kugundua kuwa miamala mbalimbali ilikuwa inafanyika kinyume na matakwa ya sheria na kanuni za usimamizi wa maduka ya fedha za kigeni na udhibiti wa utakatishaji wa haramu.
"Benki Kuu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali ilifanya ukaguzi maalum kwenye maduka yote ya kubadilisha fedha za kigeni nchini na kubaini makosa mbalimbali yaliyosababisha Serikali kusitisha leseni kwa waliokiuka Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya 36 (1)(b) na 2 (d) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2015 iliyorejewa mwaka 2019 ”, alisema Waziri huyo.
Kwa mujibu wa Chande, makosa mengine yaliyobainika ni pamoja na kutofanya utambuzi wa wateja kabla ya kutoa huduma kinyume na kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Udhibiti wa Utakasishaji Fedha Haramu, Sura 423 na kanuni ya 17 ya Kanuni za Udhibiti wa Utakatishaji wa Fedha Haramu.
"Kosa lingine lilikuwa kugawa miamala ya wateja kwa lengo la kukwepa kutunza kumbukumbu muhimu zinazoonyesha uhalali wa miamala kinyume na Kanuni ya 23 ya Kanuni za Biashara ya kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2015 na kutokutoa stakabadhi za miamala kinyume na Kanuni ya 23(1) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2015," alisema Waziri huyo.
Hata hivyo, Chande aliweka wazi kuwa wafanyabiashara watakaobanika kutokuwa na makosa watarudhishiwa fedha na mali zao.
Hadi kufikia sasa, ni maduka 68 ambayo yamefungwa huku saba yakitarajiwa kufunguliwa muda wowote.