Mamlaka ya Hali Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya uwepo wa kimbunha CHIDO katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.
Kulingana na TMA, mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kinatarajiwa kuelekea maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji kwatika kipindi cha siku nne zijazo, kuanzia Disemba 13 hadi 16, 2024.
“Kwa sasa kimbunga hicho hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja hapa nchini. Hata hivyo, kutakana na ukaribu wa maeneo ambayo kimbunga CHIDO kinatarajiwa kupita hasa kwenye eneo la kusini mwa nchi yetu, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa itakayoambatana na upepo mkali na mawimbi makubwa ya bahari kwa maeneo ya Mtwara na maeneo ya jirani,”taarifa ya TMA imesema.
Mamlaka hiyo pia imewataka watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka TMA pamoja na kupata ushauri wa miongozi ya wataalam wa kisekta.