Balozi wa tanzania nchini Uingereza, Mbelwa Kairuki./Picha: Mbelwa Kairuki IG

Serikali ya Tanzania imetoa tahadhari wake wenye nia ya kununua malori ya mizigo, huku ikiwataka kuwa waangalifu wakati wa kufanya mchakato huo.

Kupitia chapisho lake kwenye ukurasa wa X, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Mbelwa Kairuki ametoa tahadhari kwa wafanyabiashara wenye nia ya kununua malori yaliyotumika kutoka Uingereza wachukue tahadhari za msingi wanapofanya manunuzi ili kuepuka usumbufu na hasara inayoweza kutokea.

Balozi Kairuki amewataka wanunuzi hao kuhakikisha kuwa kampuni wanazotaka kufanya nazo biashara zimesajiliwa nchini Uingereza, na kwamba uhakiki huo ufanyike kupitia serikali ya Uingereza kwani hakuna malipo yoyote katika kufanya uhakiki huo.

"Ni vyema kuingia mkataba wa manunuzi na kampuni inayokuuzia lori. Wapo watanzania wanadiaspora wenye Ofisi za sheria hapa nchini Uingereza ambao wanaweza kutoa huduma ya kuandaa mkataba na hata pale inapojitokeza changamoto zozote kuwa wepesi kwa wao kufuatilia," ameshauri mwanadiplomasia huyo.

Pia amewataka wanunuzi hao kufanya upekuzi wa kufahamu historia ya malori wanayotaka kununua kabla ya kufanya malipo.

Kulingana na Balozi Kairuki, ili kufanikisha upekuzi, ni vyema kwa wanunuzi hao wapate namba za usajili ya gari zilizokuwa zimesajiliwa nchini Uingereza kabla ya kutembelea tovuti ya Serikali ya Uingereza ambapo ina mfumo wa kutoa taarifa ya historia nzima ya gari- kama liliwahi kupata ajali, limekaguliwa na kadhalika.

"Ubalozi unaamini kuwa baadhi ya njia hizo zitawasaidia wenye nia ya kununua malori kuepuka changamoto za manunuzi na usumbufu unaofuatilia katika kufuatilia kutokea mbali," ameeleza.

Kwa mujibu wa Kairuki, katika siku za karibuni ubalozi umekuwa ukipokea malalamiko ya wafanyabiashara ambao wametuma pesa zao nchini Uingereza kwa ajili ya kununua malori - lakini hawajatumiwa magari yao kwa muda unaozidi miezi 6 na wengine waliotumiwa wamepokea malori yaliyo chini ya kiwango kwa mujibu wa makubaliano.

Hali hiyo imepelekea usumbufu mkubwa na hasara kwa wafanyabiashara waliotuma pesa zao.

TRT Afrika