Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya uwepo wa kimbunga Dikeledi katika Bahari ya Hindi mwambao wa pwani ya Msumbiji.
Katika taarifa yake iliyotolewa Januari 14, TMA imesema kuwa kwa sasa kimbunga hicho hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja nchini Tanzania.
“Hata hivyo, kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo kimbunga Dikeledi kipo sambamba na maeneo ya kusini mwa nchi yetu, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika pwani ya kusini hususan katika Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa siku ya Januari 14,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Hali kadhalika, TMA imesema kuwa vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa ya Bahari vinatarajiwa kwa maeneo ya ukanda wote wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo jirani hususan kati ya tarehe 14 na 15 ya Januari 2025.
“Watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta,” TMA imesema.
Mamlaka hiyo imeongeza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga Dikeledi na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa nchini Tanzania.