Serikali ya Tanzania imesema kuwa tani 128,000 kati ya 155,000 ya sukari zimeshaagizwa hadi sasa./Picha: Getty.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Sukari Tanzania ( SBT) Profesa Kenneth Bengesi, amesema kuwa Tanzania imeendelea kuagiza sukari kufuatia mvua za El Nino zilizodhorotesha uzalishaji wa bidhaa hiyo.

"Takribani tani 128,000 kati ya 155,000 zimekwisha agizwa wakati nyengine 27,000 zipo kwenye mchakato wa kuingizwa nchini," amesema Bengesi.

Kwa mujibu wa Bengesi, serikali ya Tanzania inapanga kutathmini mahitaji ya sukari nchini humo, hivi karibuni.

Hata hivyo, Profesa Bengesi amesema kuwa bidhaa hiyo itaendelea kupatikana kwa bei ya kati ya shilingi 2,800 (dola 1.08) hadi 3,200 (dola 1.24) katika mikoa yote nchini Tanzania.

Mwezi wa pili mwaka huu, Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Bashe alisema kuwa itaendelea kuagiza sukari kutoka nje ya nchi mpaka mwisho wa mwaka 2024.

Kulingana na Waziri huyo, Tanzania ina mpango wa kuagiza zaidi ya ya tani 300,000 kupitia Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA).

Tanzania ina jumla ya viwanda saba vya sukari, vikubwa kati ya hivyo ni Kilombero, ambayo kwa siku inazalisha tani 700 za sukari, hata hivyo kiwango kimeshuka hadi 250, TPC kwa siku tani 450 lakini kwa sasa kimesimamisha uzalishaji kutoka na hitilafu za mashine, huku Kagera Sugar ikiwa na uwezo wa kuzalisha tani 500 kwa siku, lakini sasa inazalisha wastani wa tani 200 hadi 300. Viwanda vyengine ni Mtibwa na Bagamoyo, ambapo kwa mujibu wa serikali, kutokana na mvua kubwa zinazoendelea, uzalishaji umepungua kwa takriban tani elfu moja kwa siku.

TRT Afrika