Upinzani wa Tanzania ulifanya maandamano wiki jana kudai mageuzi. Picha / Reuters

Wabunge wa Tanzania wameidhinisha mageuzi ya uchaguzi licha ya malalamiko ya chama kikuu cha upinzani cha Chadema, ambacho kimeapa kupinga sheria hiyo.

Chadema inasema miswada hiyo mitatu haishughulikii matatizo ya uchaguzi uliopita wa urais mwaka 2020, ambao kiongozi wa zamani John Magufuli alishinda kwa kishindo licha ya madai ya upinzani ya kuwepo udanganyifu.

Lakini serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alichukua madaraka baada ya Magufuli kufariki mwaka 2021, inasisitiza kuwa mageuzi hayo yataboresha demokrasia katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Maelfu ya wananchi walishiriki maandamano wiki iliyopita yaliyoandaliwa na Chadema, yaliyokuwa yameitaka Serikali kufuta miswada hiyo, wakitaka uhuru zaidi kwa tume ya uchaguzi.

Kuipugia miswada kura

Wabunge walianza kujadili miswada hiyo Jumanne kabla ya kupigia kura sheria hiyo Ijumaa.

"Tumefanya kazi yetu kwa kuidhinisha miswada hiyo... Sasa tutapeleka miswada hiyo kwa Rais kwa ajili ya kuidhinisha kuwa sheria," alisema spika wa bunge Tulia Ackson.

Chadema imeelekeza ukosoaji wake hasa katika hatua ambayo ingemruhusu Rais kuteua moja kwa moja wajumbe watano kati ya 10 wa tume ya uchaguzi kabla ya uchaguzi wa rais mwakani.

Maandamano ya Chadema wiki iliyopita katika mji mkuu wa biashara Dar es Salaam yalikuwa makubwa zaidi tangu serikali ilipoondoa marufuku ya mikutano ya kisiasa ya upinzani mwaka mmoja uliopita.

"Hatujaona mabadiliko yoyote baada ya maandamano ya kwanza jijini Dar es Salaam. Badala yake, Serikali ilipuuza madai yetu na kusonga mbele na kujadili miswada yenye utata," Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliwaambia waandishi wa habari Alhamisi.

'Mageuzi ya kupambia tu'

Kiongozi wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye amekaa gerezani chini ya viongozi wote wawili, amesema miswada hiyo inatoa mageuzi ya "juu juu " tu.

Chama hicho kimetangaza kufanyika kwa maandamano ya kila wiki mwezi huu katika miji ya Mwanza, Mbeya na Arusha, kuanzia Februari 13.

Bunge linaongozwa na chama tawala cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) chenye viti 364 kati ya 392.

Rais Samia amejaribu kubadili baadhi ya sera kali za mtangulizi wake, ambaye mielekeo yake ya watu shupavu ilimpatia jina la utani "Bulldozer".

Marufuku ya mikusanyiko ya upinzani ilibatilishwa mnamo Januari 2023.

Muda mfupi baadaye, mmoja wa viongozi mashuhuri wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, alirejea nchini baada ya kukaa muda mwingi wa miaka mitano iliyopita uhamishoni.

TRT Afrika