Tume ya Madini nchini Tanzania inasema inalenga kukusanya mapato ya Shilingi Trilioni 1 sawa na dola za Kimarekani milioni 371,281,661 kutoka sekta ya madini mwaka huu.
“Mathalan katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo tulipewa lengo la kukusanya shilingi Trilioni Moja, hadi kufikia Oktoba 21, 2024 Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 312.75 ( zaidi ya dola milioni 116 ) sawa na asilimia 31.28 ya lengo la mwaka,” Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo aliwaambia wandishi wa habari.
Amesema kupitia usimamizi unaofanywa na Tume ya Madini, kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kimepanda kutoka Shilingi bilioni 624.61 ( zaidi ya dola milioni 231. 9) zilizokusanywa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.82 ( zaidi ya dola milioni 279.8) Mwaka wa Fedha 2023/2024.
Makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.7 ya makusanyo kwa miaka mitatu.
Tume imeelezea kuwa leseni za madini 34,000 zinatolewa.
Tume ya Madini pia imelezea kuwa imeweka mikakati endelevu ikiwemo kuimarisha usimamizi na udhibiti katika maeneo ya uzalishaji wa madini, ujenzi na madini ya viwandani kwa kuongeza Wakaguzi Wasaidizi wa Madini Ujenzi (AMAs), vitendea kazi (PoS) pamoja na kushirikisha Mamlaka nyengine za Serikali zinazosimamia na kutumia rasilimali hizi.
“Aidha Tume ya Madini imeendelea kusimamia kikamilifu upatikanaji wa ajira kwa Watanzania kutoka kwenye Makampuni mbalimbali ya Uchimbaji ambapo katika kipindi rejewa Kampuni ziliweza kuzalisha ajira 19,356 ambapo kati ya hizo 18,853 ni Watanzania sawa na asilimia 97.40 na 503 ni wageni sawa asilimia 2.60 ya ajira zote zilizozalishwa,”alisema Mhandisi Lwamo.
Kulingana na Tume ya Madini, jumla ya bidhaa zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 3,7 ziliuzwa na kusambazwa migodini ambapo kati ya bidhaa hizo, Kampuni za Watanzania zilifanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 3.4
Hii imeelezewa kuwa ni sawa na asilimia 91.68 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote na huduma zilizotolewa migodini.