Kiongozi Mstaafu wa chama cha ACTwazalendo,  Zitto Kabwe akizungumza wakati wa mkutano wa kuwanadi wagombea wa chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Kasulu Mjini Mkoani Kigoma. Novemba 24, 2024./Picha:  @ACTwazalendo

Serikali ya Tanzania imeitangaza Novemba 27, 2024 kuwa siku ya mapumziko ili kutoa fursa kwa raia wa nchi hiyo kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

Kwa mujibu wa tangazo namba 956 lililotolewa na serikali ya nchi hiyo, lengo ni kuwezesha watu wote wenye sifa ya kupiga kura kutumia haki yao ya kupiga kura.

Hatua hiyo pia inalenga kutoa fursa kwa Watanzania wengi zaidi kushiriki kikamilifu katika kupiga kura.

“Kwa hiyo basi, kwa mamlaka aliyopewa Rais chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa, Sura ya 35, mimi Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatoa tamko kuwa tarehe 27, Novemba 2024 itakuwa siku ya mapumziko,” ilisomeka sehemu ya tangazo hilo.

Mchakato huo, ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano, unawapa uwezo wananchi wa Tanzania kuchagua wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji pamoja na wajumbe wa halmashauri.

Pia unalenga kuimarisha uwakilishi na kuzipa jumuiya za wananchi uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi katika maeneo kama vile matumizi ya ardhi, miradi ya jamii na utoaji wa huduma.

TRT Afrika