Waziri Mchengerwa

Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa, amesema kwamba baadhi ya wagombea wa vyama mbalimbali ambao awali waliwasilisha malalamiko yao kwa mamlaka zinazohusika na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini humo hivi sasa wamerejeshwa katika nafasi zao.

Kulingana na Waziri Mchengerwa, jumla ya rufaa 5,589 kati ya 16,309 zilizowasilishwa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri nchini baada ya muda wa nyongeza wa siku mbili zilizotolewa na TAMISEMI.

“Hii ilizingatia kuwa dosari zilizokuwepo katika rufani hizo hazikuwa na madhara yeyote ya kikanuni” alisema.

Katika mkutano na vyombo vya habari jijini Dodoma, Mchengerwa amesema kuwa mbali na tathimini ya mwenendo wa zoezi la uchaguzi, mkutano huo pia unajibu kushughulikia baadhi ya malalamiko na shutuma zilizotolewa na vyama vya upinzani, ambavyo vinadai wagombea wao kuenguliwa kwa hila na wasimamizi wa uchaguzi huku Chama cha Mapinduzi CCM kikipewa nafasi ya upendeleo.

“Ili kuhakikishia haki inaendelea kutolewa na kutendekea na kanuni kufuatwa, wale wote ambao mapingamizi na rufani zao zimekidhi vigezo vya uchaguzi wamerejeshwa katika kinyan’anyiro” amesisitiza.

Aidha, amesema malalamiko yaliotolewa na vyama vya upinzani kikiwemo CHADEMA kupitia baadhi ya makada wao hayakuwa na ukweli wowote na kwamba yalilenga kuzua hofu na taharuki katika jamii.

Miongoni mwa shutuma hizo ni pamoja na zile zilizohusisha wasimamizi wa uchaguzi katika vijiji 32 vya Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani kuwaengua wagombea wote wa upinzani.

“Ukweli ni kwamba Wilaya ya Rufiji ina vijiji 38 Chadema ilimsimamisha mgombea mmoja na huku ikisimamisha wagombea wawili katika vitongoji 78 ndani ya jimbo la Rufiji na sio kweli kama walivyosema awali,” alikazia Mchengerwa.

Mchengerwa ametoa ufafanuzi huo, huku nchi hiyo ya Afrika Mashariki ikisalia na siku nne za kuanza kwa kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

Hata hivyo, mashirika na taasisi mbalimbali za kidini ikiwemo Baraza la Maaskofu wa Kanisa katoliki Tanzania (TEC) wamezitaka mamlaka husika kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki na huru.

TRT Afrika