Baada ya kukamilika, Meli hiyo ambayo pia ni maarufu kwa jina la 'Hapa Kazi Tu' ndiyo chombo kikubwa zaidi cha majini katika Ukanda wa Afrika Mashariki na itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, na mzigo wa tani mpaka 3,500, kitakapokuwa tayari kufanya kazi./Picha: Wengine

Serikali ya Tanzania imeifanyia majaribio meli ya Mv Mwanza, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya chombo hicho kitakachokua kinatoa huduma ndani ya Ziwa Victoria.

Baada ya kukamilika, Meli hiyo ambayo pia ni maarufu kwa jina la 'Hapa Kazi Tu' ndiyo kitakuwa chombo kikubwa zaidi katika Ziwa Victoria katika Ukanda wa Afrika Mashariki na itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, na mzigo wa tani mpaka 3,500, kitakapokuwa tayari kufanya kazi.

Mradi huo, unaogharimu bilioni109 (dola milioni 42.4) unatekelezwa na kampuni ya ujenzi wa meli ya Gas Entec Ship-Building Engineering Company Limited ya Korea Kusini, ikishirikiana na Kangnam Corporation, unalenga kuboresha huduma za usafiri wa majini katika ukanda wa Afrika Mashariki, kupitia chombo hicho chenye urefu wa mita 92.6 kwa 20 na upana wa mita 17, ndani ya Ziwa hilo kubwa barani Afrika.

Chombo hiko kinatarajiwa kuwa na vyumba maalumu vilivyotengwa kwa 'watu muhimu', viongozi na vyumba vya madaraja ya kwanza, huku ikianza kutengenezwa Januari 2019.

Kulingana na Erick Benedict Hamis, ambaye pia ni Meneja Mkuu wa kampuni ya Marine Services Limited, meli hiyo inatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi, hasa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa treni ya umeme ya Kisasa (SGR), ifikapo mwaka 2026.

"Kwa sasa tuko kwenye asilimia 93 ya ukamilishaji wa meli hii, hizo zilizobakia zitahusisha umaliziaji wa muonekano wa ndani wa meli, kama vile kuweka vitanda na vitu vingine," amesema Hamis.

Chombo hicho kitakuwa kinahudumu kati ya bandari za Kisumu nchini Kenya, Jinja na Port Bell (Uganda), Mwanza na Kemondo kwa upande wa Tanzania.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Sheria kutoka kampuni ya Huduma za Meli nchini Tanzania, Amina Rashid amesema majaribio yaliyofanyika yamehusisha ubora wa mitambo pamoja na kuwapa uzoefu wa majini, mabaharia na watumishi wa meli hiyo.

TRT Afrika