Na Kevin Philips Momanyi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Umewahi kujiuliza kwa nini kimbunga Hidaya kilichoikumba pwani ya Afrika Mashariki kilipewa jina hilo na ni namna gani vimbunga vinapewa majina?
Mwaka 1887, Clement Wragge, mtaalamu wa hali ya hewa kutoka Australia alianza kuvipa vimbunga majina, tena majina ya wanasiasa ambao hakuwapenda. Alitumia alfabeti za Kigiriki, au hata wanyama katika kufanikisha hili.
Mataifa mengine nayo yakaanza kuvipa vimbunga majina ya kike. Kutokana na uharibifu mkubwa unaosababishwa na vimbunga hivyo, Waziri wa Sayansi wa Australia wakati huo, Bill Morrison, alipendekeza kuwa vimbunga vipewe majina ya jinsia zote.
Baada ya hapo, vimbunga vikaanza kuwa na majina ya kiume pia.
Baada ya kuanzishwa kwake huko Geneva, Uswizi mwaka 1950, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) lilibeba jukumu la kuvipa vimbunga majina kupitia vituo vya kikanda vya hali ya hewa.
RSMC La Réunion ambayo inasimamia Kanda ya Afrika upande wa bara Hindi linashirikiana na mashirika 15 ya kitaifa ya hali ya hewa ambao wanakaa pamoja kuchagua majina ya vimbunga vinavyotarajiwa.
Jina la Hidaya lilitolewa na Shirika la Hewa la Tanzania. Kimbunga hupewa jina pindi tu kasi ya upepo inapozidi kilomita 65 kwa saa na kasi hii hurekodiwa kwa zaidi ya dakika moja, tatu, hadi kumi.
Kimbunga kinachotarajia kukumba kanda ya bara hindi kitaitwa Laly, ambacho kitafuatiwa na Jeremy, Kanga, Ludzi, Melina na kadhalika na ukiwa makini sana, utagundua kuwa majina haya yanafuata orodha ya alfabeti, yaani kila msimu majina 26 yanachaguliwa kuanzia herufi A mpaka Z.
Majina yanaweza kurudiwa baada ya miaka michache lakini kimbunga ikitokea kuwa kimbunga tajwa kinaleta madhara makubwa kuliko kawaida, basi jina lake halitotumika tena.