Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Tanzania inashika nafasi ya kwanza kati ya nchi zote za Afrika Mashariki katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari.
Kulingana na utafiti uliotolewa na Reporters Without Borders (RSF), siku ambayo dunia inaadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, Mei 3, 2024, Tanzania ni ya kwanza katika viwango vya uthabiti wa kulinda Uhuru wa Vyombo vya habari na kuweka mazingira mazuri kwa waandishi wa habari kufanya kazi.
Nchi hiyo imepanda kutoka nafasi ya 143 kwa mwaka 2023 hadi 97 mwaka huu, kulingana na utafiti huo.
"Ni habari njema sana kwa nchi yetu, ni jambo la kujivunia na hatuna budi kumpongeza na kuendelea kumuunga Rais Samia Suluhu Hassan," amesema Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania.
Nnauye amesema kuwa Tanzania imefanya vyema baada ya kukidhi vigezo vitano muhimu katika utafiti huo.
Vigezo hivyo ni pamoja na misingi ya kisheria, hali ya kiuchumi, hali ya kisiasa, usalama wa wanahabari na dhana ya kijamii na kitamaduni.
Kulingana na utafiti huo, uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umesaidia kwa kiasi kikubwa, heshima ya taaluma ya wanahabari nchini Tanzania.
Tanzania ina jumla ya magazeti 257, redio 200 na vituo vya televisheni 46. Nchi hiyo ina mitandao ya kijamii 474 na tovuti za habari 100, tangu kuanza kwa 2022, umesema utafiti huo wa RSF.
Kenya iko katika nafasi ya pili ikipanda kutoka 116 hadi 102 wakati Burundi ni ya tatu ikishika nafasi ya 108 duniani.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni ya nne, ikishika nafasi ya 123, ikifuatiwa na Uganda kwenye nafasi ya 128 ulimwenguni.
Nchi ya Sudan ya Kusini ni ya sita katika ukanda wa Afrika Mashariki na ni ya 136 duniani wakati Rwanda ni ya 144, huku Somalia ikishika mkia katika nafasi ya 145 duniani.
Serikali kushindwa kulinda wanahabari
Katika utafiti huo, RSF imeonesha kusikitishwa na kitendo cha viongozi wengi kushindwa kuwalinda waandishi wa habari.
"Serikali nyingi hazitimizi wajibu wao kikamilifu, haswa katika kuandaa mazingira wezeshi ya ufanyaji kazi wa waandishi wa habari," RSF imesema.