Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeanza jitihada za haraka za kudhibiti mamba na viboko, hatua inayolenga kunusuru maisha ya watu na mali zao.
Tayari, mamlaka hiyo imeendelea kuimarisha doria zinazoshirikisha askari wahifadhi na askari wanyamapori wa vijijini na kutoa elimu kwa jamii kuhusu jinsi ya kujikinga na kuepuka madhara yanayoweza kusababishwana wanyamapori hao.
Kulingana na Afisa Habari katika kitengo cha mahusiona kwa umma, Beatus Maganja katika kipindi cha kuanzia Januari 2024, mamba watatu na viboko wawili waliokuwa wanahatarisha maisha ya watu na mali zao waliuwawa.
Aidha, jumla ya wananchi 271, wakiwemo wavuvi 40 walipatiwa elimu juu ya kukabiliana na wanyamapori hao waharibifu.
"Hivi karibuni, kumekuwepo na ongezeko la la wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo mamba na viboko kujeruhi na wakati mwingine kusababisha vifo vya wananchi, hususan wavuvi wanaofanya shughuli zao katika bwawa la Mtera," amesema Maganja.
Kwa mujibu wa Afisa Habari huyo, hali hiyo imepelekea adha na hofu kwa wananchi wanaotegemea bwawa katika shughuli za kijamii na uzalishaji mali.
Ongezeko la matukio hayo limetokana na mvua kubwa ambazo zimeendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Tanzania na kusababisha kuongezeka kwa mtawanyiko wa wanyamapori hususan mamba na viboko kwenye maeneo ya mito na mabwawa.