Mkurugenzi wa Tume Kailima Ramadhani anasema Tume itatumia BVR zenye vifaa vinavyowasiliana ili kuchukua na kutunza taarifa za wapiga kura . / Picha TRT Afrika 

Na Ronald Sonyo

TRT Afrika, Dodoma, Tanzania

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Nchini Tanzania (NEC) imeanza kufanya maandalizi mbalimbali ikiwemo kufanya jaribio la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kuteuwa mkoa wa Tabora na Mara kwa majaribio hayo.

Hatua hii itawezesha wapiga kura ambao wameandikishwa na wapo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kuanza mchakato wa kubadili na kuboresha taarifa zao na kituo cha kupiga kura iwapo amehama wilaya ua mkoa, mwengine kurekebisha taarifa zake kwa kutumia simu ya mkononi.

Hii inamaanisha kuwa utaratibu huu hautohusu wapiga kura wapya au wale waliopoteza kadi ama kuharibika kwa kadi zao.

Vyama vya siasa nchini humo pia vitashiriki katika zoezi hilo kwa kuweka wakala kwa kila kituo cha kuandikisha wapiga kura ili kujidhirisha na hatua zinazochukuliwa na tume.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Nchini Tanzania (NEC) imeanza kufanya maandalizi mbalimbali ikiwemo kufanya jaribio la uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura/ Picha AP 

Mbali na malengo mengine zoezi hilo pia linahusisha kupima uwezo wa vifaa na mifumo ya uandikishwaji itakayotumika wakati wa uboreshaji wa datfari la kudumu la wapiga kura.

Kwa mujibu wa wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Tume Kailima Ramadhani, tume itatumia BVR kits zenye vifaa vinavyowasiliana ili kuchukua na kutunza taarifa za wapiga kura .

“Uboreshaji huo utahusisha kuandiskisha raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka18 au zaidi na atakayetimiza umri wa miaka 18 kabla au ifikapo tarehe ya uchaguzi wa mwaka 2025” alisema Kailima.

Vifaa hivyo ni tofauti na vile vilivyotumika mwaka 2015 na 2019 ambavyo zilikuwa zinatumia program ya 'Microsoft Windows' tofauti na vya sasa ambavyo vinatumia program ya 'Android.'

“Tume imesanifu na kuboresha mfumo wa uandikishaji wa kupiga kura (Votes Registration system -VRS ili kukidhi muundo wa BVR kits za sasa, ”alifafanua Kailima.

Nchi hiyo ya Afrika Mashariki inatarajia kuanza mchakato wa kufanya uchaguzi mdogo wa Serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka ujao kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.

TRT Afrika