Treni ya kisasa ya umeme nchini Tanzania (SGR)./Picha: Reuters

Mamlaka nchini Tanzania zinawashikilia watu kadhaa za kuhujumu ukusanyaji wa mapato kwa njia ya nauli zitokanazo na huduma ya treni ya umeme, maarufu kama SGR.

Kulingana na Shirika la Reli la nchi hiyo (TRC), baadhi ya abiria wanaotumia SGR wamekwepa kulipa nauli sahihi kulingana na safari wanazofanya.

Hii inafuatia uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

"Baadhi yao wamefikishwa mahakamani wakati wengine tozwa faini, mara mbili ya kiasi cha nauli walizopaswa kulipia," amesema Jamila Mbarouk, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TRC.

Licha ya kuwakamata watu hao kwa ulaghai, TRC pia imewatia hatiani baadhi ya watu wanaodaiwa kununua tiketi za treni hiyo ya kisasa kwa wingi kwa minajili ya kujipatia fedha kwa njia zisizo halali.

Kuhusu mbinu watakazotumia kudhibiti vitendo hivyo, Mbarouk ameweka wazi kuwa kwa safari zote sasa kutakuwa na ukaguzi wa tiketi wa mara kwa mara na abiria atapaswa kuchanja tiketi yake mwanzo na mwisho wa safari.

"Shirika limechukua hatua hizi ili kudhibiti vitendo viovu vya baadhi ya abiria wanaotumia treni kwa kutolipa nauli sahihi na kulangua tiketi," ameongeza.

TRT Afrika