Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na mwenzake wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier wamefanya mazungumzo ya kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kukuza ushirikiano wa kimataifa na kimaendeleo.
Mwenyeji wa ziara hiyo Rais Samia, na Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier walifanya kikao na waandishi wa habari ambapo waligusia masuala muhimu kwa uhusiano wa mataifa hayo.
"Ujerumani ni mbia wetu muhimu katika biashara na sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo maji, afya na mazingira," rais Samia alisema.
"Nchi hizi mbili zimekuwa zikishirikiana kwenye sekta mbalimbali za kimkakati hususan biashara na uwekezaji, maji, afya, usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake, uhifadhi wa bioanuai, usimamizi wa fedha, utalii pamoja na malikale na utamaduni, " Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa afrika mashariki ya Tanzania imesema.
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, yupo Tanzania kwa ziara yake rasmi ya kikazi nchini baada ya kuwasili jumatatu tarehe 30 Oktoba na kama ilivyoratibiwa, atafanya mikutano mbalimbali nchini humo.
Rais huyo alipokewa na Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa afrika mashariki, January Makamba katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.
"Uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi yetu na Ujerumani umedumu kwa zaidi ya miaka 60, na ni jukumu letu kuuendeleza na kuuongezea tija zaidi kwa manufaa ya mataifa haya mawili," amesema rais Samia. Ujerumani ni mbia wetu muhimu katika biashara na sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo maji, afya na mazingira.
Siku ya jumatano, Rais Stenmeier ataelekea mkoani Ruvuma kwa makumbusho ya Vita vya Maji Maji, ambayo ni makumbusho pekee nchini humo inayoonesha harakati za ukombozi za Tanzania dhidi ya ukoloni wa Ujerumani.