Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameongoza ibada ya watu 63 waliopoteza maisha katika maporomoko ya ardhi na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa kaskazini mwa Tanzania, huku idadi ya vifo ikitarajiwa kuongezeka zaidi.
Hata hivyo kumekuwa na takwimu za kutofautiana kutoka kwa vyanzo mbali mbali nchini humo.
Mvua kubwa iliyonyesha mwishoni mwa juma ilisomba magari na kuangusha majengo katika mji wa milimani wa Katesh, kilomita 300 (maili 185) kaskazini mwa mji mkuu Dodoma.
"Tumepoteza (watu) 63 ambao miili yao iko mbele yetu leo. Wanaume 23 na wanawake 40," Majaliwa alisema wakati wa shughuli ya kukabidhi mabaki ya wahasiriwa kwa familia zao huko Katesh.
"Tunaamini tutaokoa miili zaidi," alisema na kuongeza kuwa watu 116 walijeruhiwa katika maafa hayo.
Agizo la serikali
Wakati huo huo, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amemuagiza waziri mkuu wake Kassim Majaaliwa kusimamia shughuli za mazishi kwa wote walioathirika na kuhakikisha majeruhi wote wanapata matibabu kamili inayostahili kwa gharama ya serikali.
''Tumeelekeza serikali ya mkoa na kitengo cha maafa cha ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha kwamba wananchi wote ambao makazi yao yamesombwa na maji wapate makazi ya muda kwa ajili ya kuwastiri wananchi hao,'' imesema taarifa kwa vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, nyumba na mifugo imeathirika sana huku zaidi ya nyumba 1,150 zikisombvwa na maji na kuwaacha zaidi ya watu 5600 bila makao. Pia inakadiriwa ekari zaidi ya 750 ya mashamba imeharibiwa.
Kila kitu kilisombwa
Shughuli za utafutaji na uokoaji zilikuwa zikiendelea kwa usaidizi wa wanajeshi huku watu wakihofiwa kukwama au kufukiwa kwenye tope zito.
Picha zilizotangazwa kwenye televisheni zilionyesha vifusi kutoka kwa nyumba, ikiwa ni pamoja na samani, zikiwa zimetapakaa barabarani, huku barabara kuu, nyaya za umeme na mitandao ya mawasiliano zikiwa zimekatizwa.
Paschal Paulo, mkazi wa eneo hilo, alisema kila kitu kilikuwa kimesombwa na maji katika soko alilokuwa akifanya kazi.
James Gabriel, ambaye pia alifanya kazi katika soko hilo, alisema jamaa zake hawakupatikana na msako huo "una mfadhaiko mkubwa."
Maafa hayo yamemfanya Rais Samia Suluhu Hassan kukatiza ziara yake ya Dubai kwa ajili ya mazungumzo ya hali ya hewa ya COP28.
Tanzania na majirani zake wa Afrika Mashariki Kenya, Somalia na Ethiopia wanakabiliana na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa inayohusishwa na hali ya hewa ya El Nino.