Tanzania inasema tangazo la Umoja wa Ulaya, EU, kwamba Shirika la Ndege la Taifa la nchi hiyo, Air Tanzania liwekwa katika orodha ya ndege ambazo zimepigwa marufuku kuingia katika anga ya EU, sio marufuku.
"Shirika letu la ndege liko katika mchakato wa kushirikiana na mamlaka za Ulaya kupata kibali cha kuruka au kutua katika anga ya Ulaya," Gerson Msigwa, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania aliviambia vyombo vya habari vya nchi hiyo mwishoni mwa juma.
"Sasa hilo halipaswi kutafsiriwa kama limezuiwa," aliongeza.
Disemba 13, 2024, Tume ya Ulaya ilitoa orodha mpya inayoonyesha 'marufuku ya uendeshaji au vikwazo vya uendeshaji ndani ya Umoja wa Ulaya.'
“Air Tanzania imejumuishwa kwenye orodha. Msingi wa uamuzi huu ni masuala ya usalama yaliyotambuliwa na Wakala wa Usalama wa Anga wa Umoja wa Ulaya (EASA). Haya pia yalisababisha uamuzi wa kutoipa Air Tanzania kibali cha Opereta wa nchi ya Tatu (TCO),” imesema taarifa ya EU.
Umoja wa Ulaya unasema uamuzi wa kujumuisha Air Tanzania katika Orodha ya Usalama wa Anga ya Umoja wa Ulaya unasisitiza ‘dhamira yake isiyoyumba katika kuhakikisha viwango vya juu zaidi vya usalama kwa abiria barani Ulaya na duniani kote.’
“Tunaiomba sana Air Tanzania kuchukua hatua za haraka na madhubuti kushughulikia masuala haya ya usalama. Nimetoa usaidizi wa Tume kwa mamlaka za Tanzania katika kuimarisha utendaji wa usalama wa Air Tanzania na kufikia utiifu kamili wa viwango vya kimataifa vya usafiri wa anga,” ilisema nukuu kutoka kwa Apostolos Tzitzikostas, Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa Usafiri Endelevu na Utalii ambayo iliwekwa kwenye tovuti ya EU.
Air Tanzania yaungana na mashirika mengine 128 ya ndege ambayo yamepigwa marufuku katika anga za EU.
Air Zimbabwe ni Shirika jengine la ndege la Afrika ambalo limepigwa marufuku kama hiyo.
Katika orodha hiyo, mashirika ya ndege yaliyoidhinishwa nchini Congo Brazzaville, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Djibouti, Equitorial Guinea , Eritrea, Liberia, Libya, São Tomé na Príncipe, Sierra Leone na Sudan yamewekwa kwenye orodha ya marufuku.
EU inasema hii ni kutokana na 'usimamizi duni wa usalama wa mamlaka ya usafiri wa anga kutoka Mataifa hayo.'
Maamuzi hayo yalifanywa na maoni ya pamoja ya wataalamu wa usalama wa anga wa Jimbo la Wanachama, ambao walikutana Brussels mnamo 19 hadi 21 Novemba 2024 chini ya Kamati ya Usalama ya Anga ya EU.
Kuamua kama kupiga marufuku au kutopiga marufuku shirika la ndege EU inasema, inategemea tathmini inayofanywa dhidi ya viwango vya usalama vya kimataifa.
Hii inachukuliwa kutoka kwa mashirika tofauti. Hii ni pamoja na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), Utawala wa Usafiri wa Anga wa Marekani, Wakala wa Usalama wa Anga wa Umoja wa Ulaya (EASA).
Pia inategemea ripoti za ukaguzi kwenye ndege zinazotumiwa na waendeshaji wa nchi za tatu (SAFA) na ripoti za Waendeshaji wa Nchi tatu, pamoja na taarifa iliyokusanywa na Nchi Wanachama wa Umoja wa Ulaya na Tume ya Ulaya yenyewe.
Inasema tathmini hii inafanywa dhidi ya viwango vya usalama vya kimataifa. Marufuku hiyo pia inaweza kutekelezwa kwa mashirika ya ndege ndani ya Umoja wa Ulaya na inatumika tu kwa usafiri wa anga wa kibiashara na wa mizigo.
Safari za ndege za kibinafsi na zisizo za kibiashara haziathiriwi. Shirika la ndege, kupitia pendekezo na kwa Tume ya Ulaya linaweza kuomba kuondolewa kwenye orodha ya marufuku ikiwa itathibitisha kuwa limefikia viwango vya usalama vya kimataifa.
Huduma za Tume ya Ulaya kisha zitatathmini ushahidi, Tume ya Ulaya itapendekeza kuondolewa kwa Kamati ya Usalama wa Anga ya EU.
Msigwa, amewahakikishia Watanzania kuwa nchi bado inafuata taratibu zinazostahili kufikia anga za Umoja wa Ulaya, na hii itachukua muda.
“Wataalamu kutoka mamlaka zinazosimamia anga ya Ulaya wapo Tanzania na wanaendelea kujadiliana na mamlaka za Tanzania ili kufikia hatua ambayo Shirika letu litaanza kuingia katika anga ya Ulaya," amesema Msigwa.