Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) imebainisha upungufu wa majaribio ya ulaghai kwa njia ya simu katika robo ya mwaka iliyoishia Septemba 2024 na Disemba 2024.
Ripoti hiyo pia inaonesha mikoa ya Rukwa na Morogoro ikiongoza kwa kuwa na zaidi ya theluthi moja ya majaribio yote ya ulaghai kwa njia ya simu nchini Tanzania.
Wakati mkoa wa Rukwa ukiwa na majaribio 5,305, Morogoro ilikuwa na matukio 4,278 huku Mbeya ikishika nafasi ya tatu na majaribio 930.
“Rukwa na Morogoro ziliongoza kwa kuwa na majaribio mengi ya ulaghai ikifuatiwa na Mbeya, Dar es Salaam na Katavi,” imesomeka sehemu ya takwimu hiyo.
Kwa upande mwingine, Mikoa ya Kusini Unguja, Kusini Pemba na Kaskazini Pemba ilikuwa na idadi ndogo ya majaribio ya ulaghai.
Kwa ujumla, maeneo hayo tajwa yalikuwa na majaribio 28 ya ulaghai kwa mujibu wa TCRA.
Pamoja na mambo mengine, takwimu hiyo pia ilitoa mwenendo wa mawasiliano ya simu, pesa mtandao, Intaneti, utangazaji, posta na usafirishaji wa vifurushi na vipeto.
Takwimu hizo zimeandaliwa kwa kuzingatia viwango vya Umoja wa Mawasiliano Duniani (ITU) vya kukusanya na kuandaa takwimu za huduma ya mawasiliano/TEHAMA.