Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania./Picha: Getty

Kuingia madarakani kwa Rais Samia Suluhu Hassan, hasa baada ya kifo cha ghafla cha mtangulizi wake John Pombe Magufuli, mwezi Machi 2021, kulidhihirisha uhai mpya kwa tasnia ya habari ambayo ilikuwa mahututi hapo awali.

“Nawaambia wamiliki wa vyombo vya habari, kuweni makini. Kama mnafikiri mna uhuru, sio kwa namna hiyo," aliwahi kunukuliwa Rais Magufuli.

Baadhi ya Watanzania wakisoma magazeti nchini humo./Picha: Reuters

Enzi mpya

Hata hivyo, mara baada ya kuingia kwa Rais Samia Suluhu Hassan, vyombo vya habari Tanzania vilianza kuona ahueni fulani kwenye tasnia hiyo.

Mwezi Aprili 2021, Rais Samia alivitoa kifungoni vyombo vya habari ambavyo vilifungwa na mtangulizi wake, uamuzi ambao ulipokelewa kwa furaha na Taasisi ya Kimataifa ya vyombo vya habari (IPI).

“Nimesikia kuwa kuna baadhi ya vyombo vya habari vimefungiwa. Vifunguliwe, tusitoe nafasi ya watu kusema kuwa tunakandamizi uhuru wa vyombo vya habari, tuhakikishe tu kuwa vinafuata sheria zilizowekwa,” alinukuliwa Rais Samia.

Mwezi Aprili 2021, Rais Samia alivitoa kifungoni vyombo vya habari ambavyo vilifungwa na mtangulizi wake, uamuzi ambao ulipokelewa kwa furaha na Taasisi ya Kimataifa ya vyombo vya habari (IPI)./Picha: Wengine

Dalili za mapema

Hata hivyo, mambo yalianza kubadilika taratibu na dalili za mapema zilianza kujidhihirisha.

Agosti 2021, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alisitisha uchapishaji wa Gazeti la Uhuru kwa muda wa siku saba. Gazeti hilo linamilikiwa na chama tawala cha nchini Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Uamuzi huo ulitokana na gazeti hilo kuandika habari isiyo sahihi inayodai kwamba Rais Samia Suluhu Hassan hana nia ya kugombea urais mwaka 2025. Mwezi mmoja baadae, serikali ya Tanzania ilisitisha uchapishaji wa gazeti la Raia Mwema kwa siku 30 kuanzia Septemba 9, 2021.

Serikali ya Tanzania ilifikia hatua hiyo kwa kudai kwamba gazeti hilo lilikiuka maadili ya uandishi wa habari mara kwa mara.

Mwezi Agosti 2024, TCRA ilitoa onyo kali kwa Watetezi TV kwa kurusha habari zinazodaiwa kuwa za kichochezi kupitia chaneli yake ya YouTube, ikisema kuwa licha ya kituo hicho kuandikiwa barua ya onyo tarehe 5 Aprili 2024, kimeendelea kukiuka Sheria, Kanuni, na Masharti ya Leseni kwa kurusha tena maudhui yanayokinzana na sheria tarehe 30 Julai 2024.

Katika taarifa yake iliyotolewa Oktoba 2, ambayo pia ilitoa hukumu kwa Mwananchi Communications Limited, TCRA ilidai kuwa maudhui yaliyochapishwa na kampuni hiyo, yalileta tafsiri hasi kwa Tanzania, jambo ambalo linaathiri na kuharibu umoja, amani na mshikamano wa kitaifa.

TRT Afrika