Kulingana na ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), asilimia 32.13 ya Watanzania wanatumia 'Simu janja'./Picha: Wengine

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii nchini Tanzania wanaitaka Serikali kupunguza kodi ya uingizwaji wa 'simu janja' ili kuongeza wigo wa umiliki wa vifaa hivyo vya kisasa.

Wadau hao wanasema kuwa gharama kubwa za vifaa hivyo zinawanyima Watanzania wengi fursa za kumiliki simu hizo ambazo zinatawala sehemu kubwa za maisha yao ya kila siku.

"Serikali imefanya vyema katika kuweka miondombinu ya kutosha katika eneo la Teknolojia, Habari na Mawasiliano, hata hivyo ni vyema zaidi ikafuta kodi kwenye bei za vifaa hivi," anasema Deus Kibamba, mchambuzi wa masuala ya Kisiasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania.

Kulingana na Kibamba, hakuna haja na kuwa na sera na miongozo ambayo haimuwezeshi Mtanzania wa kawaida kuweza kumiliki 'Simu Janja'.

"Maeneo mengi ya vijijini nchini Tanzania yana miundombinu ya kuridhisha ya mawasiliano, lakini itakuwa haina tija kama haimnufaishi mwananchi wa kawaida," anaielezea TRTAfrika.

Kibamba anaongeza kuwa Watanzania wengi wanakosa fursa adimu na huduma muhimu zinazopatikana mitandaoni kutokana na matumizi duni ya 'Simu Janja'.

Katika ripoti yake ya robo ya nne ya mwaka ya hivi karibuni, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inasema kuwa ni asilimia 32.13 tu za simu hizo za kisasa ziko katika matumizi nchini.

"Hadi kufikia Disemba 2023, matumizi ya simu zote yamefikia asilimia 85.62, lakini yale ya simu janja yameongezeka kutoka asilimia 30.71 hadi kufikia 32.13," inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Kulingana na mdhibiti huyo wa huduma za mawasiliano nchini Tanzania, asilimia 67.8 ya watanzania waishio mijini wanapata huduma za intaneti ukilinganisha na asilimia 28.9 ya waishio maeneo ya vijijini.

Katika ripoti yake ya robo ya nne ya mwaka ya hivi karibuni, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inasema kuwa ni asilimia 32.13 tu za simu hizo za kisasa ziko katika matumizi nchini./Picha: Wengine

Kwa upande wake, mwanaharakati na mchambuzi wa mambo ya Kijinsia nchini Tanzania, Deogratius Temba anashangazwa kuona matumizi madogo ya 'Simu Janja' wakati dunia inajiandaa na wimbi la Akili Mnembo(AI).

"Matumizi ya Simu za kisasa hayaepukiki kwa sasa, hususani wakati kila huduma inatolewa kwa njia ya intaneti," Temba anasema.

Mchambuzi huyo anaiomba serikali kukaa chini na makampuni ya simu na kuzipitia kodi kubwa zinazotozwa katika uingizaji wa vifaa hivyo vya kisasa, ili kuhakikisha kuwa Watanzania wengi zaidi wanazimiliki.

TRT Afrika