Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, TCRA, Dkt. Jabiri Bakari./Picha: TCRA

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imelifungia Gazeti la Mwananchi na The Citizen kuchapisha habari mtandaoni kwa muda wa siku 30.

Kwa mujibu wa TCRA, hukumu hiyo imetolewa baada ya kampuni ya Mwananchi Communications, inayomiliki mitandao ya kidijitali ya The Citizen na Mwananchi, kuchapisha maudhui yanayokiuka kanuni za maudhui ya Mtandaoni za mwaka 2020.

Katika taarifa yake kwa umma, iliyotolewa Oktoba 2, 2024, TCRA inadai kuwa mnamo tarehe 1 Oktoba, 2024, Mwananchi Communications Limited ilichapisha maudhui mjongeo na sauti kwenye mitandao yake ya jamii, maudhui yaliyozuiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 16 ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni zilizorejewa.

Kulingana na TCRA, maudhui hayo yameleta tafsiri hasi kwa Tanzania, jambo ambalo linaathiri na kuharibu umoja, amani na mshikamano wa kitaifa.

“Umma unataarifiwa kuwa, kufuatia kuchapishwa kwa maudhui yaliyokatazwa na yanayopingana na sheria, TCRA imesitisha kwa muda leseni za huduma za maudhui mitandaoni za Mwananchi Communications Limited (The Citizen, Mwananchi Digital, Mwananchi na Mwanaspoti) kutoa huduma za maudhui mitandaoni nchini Tanzania kwa muda wa siku 30 tangu kutolewa kwa taarifa hii, wakati masuala mengine ya kiusimamizi yanafanyiwa kazi,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

TRT Afrika