Idadi za televisheni za mtandaoni nchini Tanzania zimepungua kutoka 231 hadi 215, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema katika ripoti yake ya robo mwaka.
Kulingana na TCRA, wamiliki wa leseni za televisheni za mtandaoni wamepungua kwa asilimia 7.4.
Upungufu huo umeshuhudiwa kati ya mwezi Machi hadi Juni 2024, kwa mujibu wa TCRA.
Kwa sasa, gharama za usajili wa televisheni za mtandaoni nchini Tanzania ni Dola 184 (Shilingi 500,000) kutoka Dola 369 (1,000,000), iliyokuwa awali.
Wakati huohuo, TCRA imesema kuwa majaribio ya ulaghai yameongezeka kwa wastani wa asilimia 57, huku kukiwa na 22, 257 hadi kufikia mwezi Juni, 2024.
"Mikoa ya Rukwa na Morogoro ndiyo inayoongoza, ikiwa na zaidi ya theluthi moja ya majaribio yote ya ulaghai nchini. Mbeya, Dar es Salaam na Arusha zinafuata kwa majaribio ya ulaghai kwa zaidi ya 1 hadi 10," TCRA imesema.
Mikoa mingine ya Kaskazini Pemba, Kusini Unguja na Kusini Pemba ina idadi ndogo ya majaribio. Kila mkoa ulirekodi asilimia 0.01.
Kulingana na TCRA, hali ya mawasiliano katika robo inayoishia Juni 2024 imeonesha maendeleo makubwa kwa kuongezeka kwa utumiaji wa huduma za mawasiliano, ikichochewa na ushindani endelevu wa bei za huduma. Moja ya mafanikio hayo ni kuenea kwa mtandao wa simu za mkononi katika teknolojia mbalimbali, ambapo mtandao wa 3G umeenea kwa asilimia 89 ya watu, na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma ya Intaneti.