Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) yashindwa kuendesha kesi kutokana na ukosefu wa fedha

Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) yashindwa kuendesha kesi kutokana na ukosefu wa fedha

Katika tangazo lake kwa umma, Mahakama ya EACJ imesema imelazimika kusitisha usikilizwaji wa kesi kwa mwezi Juni 2024
Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki(EACJ) ikiwa katika moja ya vikao vyake jijini Arusha, Tanzania./Picha: EACJ-X

Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) itashindwa kusikiliza kesi kwa mwezi wa Juni, 2024 kutokana na ukosefu wa fedha.

Katika taarifa yake kwa umma, Mahakama hiyo inayoketi jijini Arusha, Tanzania , EACJ imesema italazimika kusitisha kusikilizwa kwa mashauri mbalimbali kutokana na ukata.

"Kutokana na michango duni kutoka kwa nchi wanachama, Mahakama ilishindwa kuendesha shughuli zake za mwezi Mei 2024 na mwezi Juni," ilisomeka sehemu ya taarifa ya Mahakama hiyo.

Kulingana na EACJ, changamoto hiyo ya kifedha inatatiza shughuli za utoaji haki ambayo ni moja ya majukumu ya mahakama hiyo.

"Kwa hali hiyo, kumekuwa na mrundikano mkubwa wa kesi, huku zaidi ya mashauri 200 yakisubiri kutolewa maamuzi," iliongeza.

EACJ ilianzishwa mwaka 2001 ikiwa na jukumu la kuhakikisha kuwa sheria zote ndani ya nchi wanachama zinatafsiriwa kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.

Pia hutoa maoni na ushauri wa kisheria, pamoja na kujihusisha kwenye usuluhishi.

TRT Afrika