Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania kimeitaka kampuni ya mawasiliano ya Tigo kujibu shutuma za mfanyakazi wa zamani; kuwa kampuni hiyo ilisaidia serikali kufuatilia eneo la mpinzani wake ambaye baadaye alishambuliwa katika jaribio la kumuua lililoshindikana.
Mfanyakazi wa zamani wa kampuni mama ya Tigo, Millicom, aliiambia mahakama ya Uingereza mwezi huu kwamba Tigo ilishiriki data ya simu ya mkononi na serikali inayoonyesha eneo alipo mbunge wa upinzani Tundu Lissu wiki chache kabla ya shambulio hilo.
Gari la Lissu lilishambuliwa kwa risasi Septemba 2017 na watu wasiojulikana, kwa mujibu wa faili za mahakama zilizoonekana na Reuters.
"Nimemfahamisha (wakili) Bob Amsterdam leo kuanza kesi dhidi ya Tigo na serikali ya Tanzania," Lissu aliambia mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa hana imani na mahakama za ndani kushughulikia kesi hiyo.
Kampuni inakanusha madai
"Tutawalazimisha Tigo watuambie walikuwa wanawasiliana na nani. Nani kutoka serikalini aliwataka wanifuatilie kwa saa 24. Ni lazima watuambie majina."
Katika majalada yake ya mahakama mwezi huu, Millicom ilisema imepata habari mwishoni mwa Agosti au mapema Septemba 2017 "kuhusu data ya simu ya rununu ya mwanasiasa wa eneo hilo kutumwa kwa wakala wa serikali."
Ilisema watu waliohusika walikuwa na nidhamu na mafunzo ya ziada yalitolewa kwa kampuni tanzu za Millicom kuhusu jinsi ya kujibu maombi ya data ya kampuni.
Kampuni hiyo ilikanusha madai katika kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mfanyakazi wake, Michael Clifford, kwamba Clifford amefukuzwa kazi kwa sababu ya kuibua wasiwasi kuhusu ufuatiliaji wa data za eneo la alipokuwepo Lissu.
Bado hakuna aliyekamatwa
Kesi hizo ziliripotiwa kwa mara ya kwanza Jumanne na gazeti la Uingereza la The Guardian.
Wasemaji wa Millicom na serikali ya Tanzania hawakujibu au kutoa maoni yoyote wakati chombo cha habari cha Reuters kilipowasiliana nao siku ya Jumatano.
Rais wa wakati huo wa Tanzania John Magufuli alilaani shambulizi dhidi ya Lissu mwaka 2017.
Hakuna aliyekamatwa au kufunguliwa mashtaka kuhusiana na tukio hilo.
Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alimrithi Magufuli baada ya kifo chake mwaka 2021, aliahidi kuondoa vikwazo dhidi ya wakosoaji wa serikali vilivyowekwa na Magufuli, lakini mashirika ya kutetea haki yanasema mamlaka imekuwa ikiwalenga wapinzani kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Desemba.
Serikali imekanusha tuhuma hizo. Jumatatu, Lissu alikuwa miongoni mwa viongozi kadhaa wa upinzani waliokamatwa kwa muda mfupi na polisi kabla ya kuandamana kupinga kile walichosema ni mauaji na kutekwa nyara kwa wakosoaji wa serikali.