Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa jitihada zaidi zitawekwa kuwalinda watu dhidi ya mashambulizi ya tembo.
Alliwaambia wananchi wa Tarafa ya Matemanga Wilaya ya Tunduru kuwa Serikali itaendelea kupeleka ndege nyuki katika Wilaya za Namtumbo na Tunduru ili kutatua tatizo la ndovu wanaoshambulia mazao ya wananchi.
Amesema tatizo hili amelisikia tangu atembelee eneo la Namtumbo.
"Na ndege nyuki tulio nayo mpaka sasa nadhani ni hiyo moja au mbili, kwa hiyo itakuwa inakuja inafanya kazi inaondoka inakwenda kuhudumua kwengine. Lakini naahidi hali ikiwa mzuri tutaongeza ili ziwe nyingi kuweza kuhudumia wananchi," aliongeza kusema Rais Samia.
Nchini Tanzania, baadhi ya jamii zenye changamoto ya kuvamiwa na tembo wamebuni mbinu kadhaa za kuwafukuza.
Wengine wamechukua hatua ya kujaza mpira na unga wa pilipili - kiungo ambacho tembo wanakichukia.
Wengine hutumia sauti kama njia ya kuwafukuza, wakipiga kwa sauti kubwa ndoo za chuma katika vipindi fulani ili kuwatisha tembo.
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inasema kati ya Januari 2023 na Julai 2024, takriban tembo 500 waliovamia makazi ya watu walirudishwa kwa lazima kwenye mapori na mbuga za wanyama.
Mwezi Mei mwaka huu, Wizara ya Maliasili na Utalii ilitangaza hatua za kudhibiti migogoro ya binadamu na wanyamapori, hasa mashambulizi ya tembo.
Kwa mujibu wa Wizara hiyo, hatua hizo ni pamoja na kuajiri walinzi wapya 1,187 katika kipindi cha miaka miwili ijayo ili kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori na kudhibiti wanyamapori kuvamia maeneo ya makazi.
Wizara ilisema itapeleka askari wa wanyamapori TAWA, Hifadhi za Taifa Tanzania, na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.