Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile ni kiongozi mashuhuri wa Afrika, mwanasiasa, mwanasayansi na mtaalam wa afya ya umma aliye na uzoefu mkubwa wa kiufundi na majukumu ya sera./ Picha: TRT Afrika

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizowasilisha pendekezo la mgombea wa nafasi ya Mkurugenzi wa Afrika wa Shirika la Afya Duniani WHO.

Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile, aliyependekezwa na Tanzania, alikuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa nchi hiyo kati ya Disemba 2020 na Septemba 2021 na pia amewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya.

Ndugulile atawania nafasi hio pamoja na wagombea wengine wanne kutoka kanda mbali mbali za Afrika.

Mshindi atachukua nafasi ya Dkt Matshidiso Moeti wa Botswana, ambaye amehudumu kwa mihula miwili katika nafasi hiyo na hastahili kuchaguliwa tena.

Moeti, ambaye aliteuliwa mnamo 2015, amesimamia shughuli za WHO kupitia hali ngumu, pamoja na milipuko ya Ebola na janga la COVID-19.

Dkt Matshidiso Moeti wa Botswana, amehudumu kwa mihula miwili katika nafasi ya Mkurugenzi wa WHO Afrika na hastahili kuchaguliwa tena/ Picha: Reuters 

Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile ametaja katika manifesto yake kuwa akiteuliwa ataleta uongozi uliokamilika katika nyanja zote ili kufanikisha miradi ya afya barani Afrika kwa wepesi zaidi.

''Mengi yamefanikiwa na hatua kupigwa katika kufikia malengo kadhaa ya maendeleo ya Millenia,'' amesema Ndugulile. ''Sasa tunahitaji kiongozi ambaye atakuwa na mtazamo tofauti, ambaye anajumuisha ujuzi wa kiufundi, sera za kisiasa ili kutia nguvu na kuwa na msukumo wa mwisho kuelekea malengo ya SDG,'' Dkt Ndugulile ameambia TRT Afrika.

Kwa mujibu wa Dkt Ndugulile, WHO Afrika inahitaji kuweka upya kipaumbele katika ujumuishaji wa kisiasa, hivyo kuwa na mtazamo chanya wa kisiasa na jumuishi pamoja na uongozi wa kiufundi utakaojenga uwezo wa utafiti wa kikanda na afya ya umma.

''Ninalenga maeneo manne ya uwekezaji kwa kipaumbele: Kuwezesha haki ya afya, kuwezesha utayari wa janga la afya endapo litatokea, kuainisha siasa za maendeleo katika sekta ya afya na kuundwa kwa ofisi thabiti ya Afrika ya WHO itakayokuwa na athari kubwa kwa afya ya bara,'' amesema Dkt Ndugulile.

Wasifu wa masomo wa Dkt Ndugulile

Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile ni kiongozi mashuhuri wa Afrika, mwanasiasa, mwanasayansi na mtaalamu wa afya ya umma aliye na uzoefu mkubwa wa kiufundi na majukumu ya sera.

Ana Shahada ya Daktari wa Tiba (MD) na Shahada ya Uzamili ya Dawa (MMED) katika Mikrobiyolojia ya Afya na taaluma ya kinga ya maradhi kutoka kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shahada ya Uzamili ya Afya ya Umma (MPH) kutoka Chuo Kikuu cha Western Cape, na Shahada ya Kwanza ya Sheria (LL.B) kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Pia Dkt. Ndugulile ni Makamu Mwenyekiti wa Ushauri wa Kamati ya Afya katika Umoja wa Mabunge (IPU), na ni mwanachama wa Kamati Tendaji ya Mtandao wa Kamati za Afya za Bunge la Afrika (NEAPACOH) miongoni mwa majukumu yake mengi katika vyombo vya kimataifa.

Wagombea kutoka maeneo mengine Afrika

Wagombea wengine kwa nafasi hiyo kubwa zaidi ya WHO barani Afrika ni:

Dkt. Ibrahima Socé Fall kutoka Senegal, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa WHO anayesimamia magonjwa ya kuambukiza yaliyotelekezwa (NTD).

Dkt. N'da Konan Michel Yao, aliyependekezwa na nchi yake ya Côte d'Ivoire, amekuwa Mkurugenzi wa Operesheni za Afya za WHO tangu Agosti 2020, ambapo anaratibu mwitikio wa mwili kwa majanga ya kiafya, asili na ya kibinadamu.

Dkt. Richard Mihigo, kutoka Rwanda, pia yuko Geneva ambako amefanya kazi katika taasisi ya chanjo barani Afrika, Gavi tangu 2022. Hivi sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimkakati na Umoja wa Afrika na Afrika CDC. Kabla ya hili, alikuwa kiongozi wa kimataifa wa Gavi na Mkurugenzi Mkuu wa Utoaji wa Chanjo ya COVID-19, Uratibu na Ushirikiano.

Dkt. Boureima Hama Sambo, wa Niger, ni Mwakilishi wa WHO katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kama Mkuu wa Ujumbe. Hapo awali amefanya kazi katika makao makuu ya WHO kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.

Kamati ya Kikanda ya WHO Kanda ya Afrika itampigia kura ya siri mkurugenzi wa kanda ajaye katika mkutano kuanzia tarehe 26 – 30 Agosti huko Brazzaville katika Jamhuri ya Congo.

TRT Afrika