Na Sylvia Chebet
Watu wengi hukosa utulivu kutokana na harafu mbaya za vinywa.
Matatizo haya ni kawaida sana na husababisha meno kuoza.
Magonjwa ya vinywa huathiri karibu watu bilioni 3.5, kulingana na Shirika la Afya Duniani.
Ili kuepuka kadhia za aina hii, baadhi ya watu hupiga mswaki mara kwa mara, kwa kutumia nguvu na kugusa sehemu hatarishi kwenye vinywa vyao.
Baadhi ya makosa ya kawaida katika afya ya kinywa:
Kushindwa kupiga mswaki kwa usahihi
Unaweza kudhani kuwa unapiga mswaki kwa usahihi kwa kuwa umekuwa ukifanya hivyo kwa miaka mingi. La hasha.
Akizungumza na TRT Afrika, Dkt Radhia Okumu, anaweka wazi kuwa "anashuhudia watu wengi wakitembelea kliniki yake mjini Nairobi kutokana na matatizo ya vinywa.”
Safari za mara kwa mara hospitalini sio suluhisho, kulingana na wataalamu wa afya.
Madaktari wa meno wanapendekeza kushikilia mswaki kwa pembe ya nyuzi 45 karibu na mstari wa fizi ili kuondoa utando ambao unaweza kusababisha ugonjwa wa fizi.
Makosa ya kawaida wakati wa kupiga mswaki ni kutumia nguvu. Wakati mwingi, watu hupiga mswaki kwa nguvu na kwa haraka sana, wakidhani ni njia sahihi ya kung'arisha meno yao.
Dkt Okumu anasema watu wengi kufanya hivyo ni kung'arisha meno, bila kufahamu athari wanazozipata.
“Inaharibu meno kwani huondoa sehemu ya tabaka kwenye meno.”
Kulingana na wataalamu wa afya za kinywa, ni miswaki milaini pekee yenye kufanya kazi kwa ufanisi.
Mbali na meno, ni vizuri pia kusafisha ulimi ili kuondoa harufu mbaya, hali inayoathiri asilimia 25 ya watu duniani.
“Pia, tunakatakiwa kupiga mswaki kwenye pande zote za mashavu. Na ndio maana nasisitiza matumizi ya miswaki laini.”
Kusukutua
Kila mara baada ya kupiga mswaki watu wengi husukutua midomo yao ili kuondoa mabaki ya dawa kwenye meno yao.
Hii haifai, kulingana na Dkt Okumu ambaye anashauri "kutema mate tu bila kusukutua.”
"Kwa kawaida, unatakiwa kusuuza kinywa chako kabla ya kupiga mswaki ili floridi hiyo isalie mdomoni," anaongeza.
Dkt Okumu anapendekeza umuhimu wa kusubiri walau nusu saa baada ya kupiga mswaki ikiwa watatumia viosha vinywa..
Usichokonoe meno kila siku
Wataalamu wanasema kuchokonoa meno ni sehemu muhimu ya usafi wa kinywa ambayo husafisha mabaki ya chakula yaliyonasa kwenye mianya, hata hivyo inapaswa kufanyika walau mara moja kwa siku.
Kuchokonoa meno mara kwa mara huongeza hatari ya kuendeleza matatizo ya meno kutokana na ukuaji wa bakteria hatari.
"Mengi ya mashimo ambayo kwa kawaida tunakumbana nayo, yako kati ya meno, sio juu sana kwa sababu nadhani tunafanya kazi nzuri juu, lakini hatufanyi kazi ya kuchokonoa chochote katikati," anabainisha Dkt Okumu.
Kulingana na tafiti, mswaki husafisha kinywa kwa asilimia 60, wakati uchokonoaji wa meno hufanya asilimia 40.
Watu wengi hupenda kutumia viosha vinywa badala ya kusugua. Ingawa inasaidia kuua vijidudu, haitoi chembe za chakula zilizobaki katikati.
Vyakula vyenye sukari na asidi
Sukari nyingi hudhuru meno ikiwa hayajasafishwa mara baada ya matumizi yake. Kunywa maji mara moja kunaweza kusaidia kuiondoa sukari.
Matumizi ya limao yaliongezeka sana wakati wa Uviko 19, lakini wataalamu wa afya ya kinywa wanaonya juu ya matumizi yaliyopitiliza.
“Limau ina asidi na huharibu kutu."
Kulingana na Dkt Okumu, ikiwa ni lazima kunywa maji ya limao kila siku, tumia majani ili kuepuka kugusana na meno.
Madaktari pia wanapendekeza kwamba watu wanywe maji mengi. Mara tu mdomo wako unapokuwa na maji, una nafasi ndogo ya kupata matundu, Dkt Okumu anasema.
"Maji ni ya muhimu sana kwa sababu huosha chembe za chakula na pia hupunguza asidi mdomoni."
Pia anapendekeza matumizi ya jibini ambayo vile vile hupunguza asidi, kwani huongeza mate kwenye kinywa.
Madaktari wanashauri kuacha kuvuta sigara ili mtu awe na afya nzuri ya kinywa.
"Uvutaji sigara sio mzuri kwa afya yako. Sio mzuri kwa meno kwa sababu ya nikotini."
Kutokwenda kwa daktari wa meno
Hutohitaji kwenda kumuona daktari wa meno ikiwa unapiga mswaki na kusafisha kinywa chako kila siku.
Ni muhimu kuweka miadi na daktari wa meno, walau mara moja kwa mwaka.
Kumuona daktari kunaweza kusaidia kutambua mapema na kutibu matatizo ya meno. Kwa wale walio na historia ya matatizo ya meno, ni muhimu kupanga kumuona daktari wa meno mara nyingi zaidi.
Ni muhimu kujali afya za vinywa vyetu.