Na Lulu Sanga
Mjadala wa uraia pacha umepamba moto katika kila mtandao wa kijamii nchini Tanzania. Hii imetokana na kauli ya serikali ya Tanzania hivi karibuni kuwa takriban raia 66 wa Tanzania wameukana uraia wa nchi hiyo na kupewa hadhi ya uraia katika nchi nyingine.
Hata hivyo nchi hiyo ya Afrika mashariki imefafanua kuwa bado haipo tayari kuruhusu suala la uraia pacha nchini humo.
Kupitia waziri wa mambo ya nje ya nchi Stergomena Tax Tanzania imejipanga kuwapatia diaspora wenye asili ya Tanzania hadhi maalumu itakayo wawezesha kufanya shughuli za kiuchumi nchini Tanzania.
Hata hivyo mpango huu wa Tanzania umepokelewa kwa hisia tofauti na diaspora wa Tanzania wanaoishi ughaibuni ambapo baadhi wameipongeza hatua hiyo huku wengine wakisisitiza suala la hadhi maalumu kuwa ni jambo linaloweza kubadilishwa wakati wowote na kiongozi yoyote anayeingia madarakani.
Mwenyekiti wa Baraza la Diaspora Tanzania, Bupe Amon Kyelu, anautaja utafiti uliofanywa na taasisi hiyo kuwa umebaini kuwa wahamiaji wengi wanaoishi katika mataifa ambayo hayaruhusu uraia wa nchi mbili kwa wakati huu kupata hadhi maalum waliyopewa na nchi yao kuwa ni suluhisho la haraka.
“Hivi sasa hadhi maalum inaweza kuwa suluhu kwa sababu suala la uraia pacha halijakubalika duniani kote, na hata ikiruhusiwa Tanzania baadhi ya wanadiaspora ambao tayari ni raia wa nchi nyingine ambazo hawajakubali uraia pacha watakuwa na wakati mgumu, ikiwa ni pamoja na kupoteza haki zao katika nchi hizo,” anaeleza Bupe.
Madhumuni na mipaka
Hata hivyo ameiambia TRT kuwa hofu ya baadhi ya Watanzania kwamba mtu mwenye uraia wa nchi nyingine bado anaweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kitaifa nchini Tanzania, ikiwamo uchaguzi, kwa kiasi kikubwa haina msingi.
"Hilo sio lengo," anasema. “Tunataka hadhi hii maalum itusaidie katika mambo ya msingi kama vile vitambulisho maalum, uhuru wa kurudi nyumbani Tanzania bila kuomba viza, uwekezaji na watoto kurithi mali za nyumbani, zaidi tunaleta maarifa tuliyoyapata nje ya nchi", anasisitiza Bupe
Kulingana na Bupe, athari za kikatiba za hadhi maalum kwa wanaoishi nje ya nchi, na kama hii inaweza kuingiliana na haki za kisiasa, kwa sasa hata haliko katika majadiliano.
“Suala la kupiga kura au kugombea nafasi za kisiasa si suala la mjadala kwa sababu ni suala la kikatiba,’’ Mwenyekiti wa baraza la diaspora anasema.
Bupe anaona hadhi maalum kama hatua ya kwanza tu, akisisitiza kwamba katika siku za usoni, suala la uraia wa nchi mbili litarudi.
"Tunaamini kama serikali ilivyoahidi tutapata sifa ya pekee, lakini kizazi kijacho kitahitaji uraia pacha kwa kuwa mambo yanabadilika, kunaweza kuwa na mabadiliko ya sera ya uongozi, na ni suala pana la kisiasa, hatujakata tamaa," anasema.
Kwanini baadhi ya nchi hazipo tayari kuruhusu uraia pacha?
TRT Afrika pia imezungumza na Godwin Gonde Godwin Gonde, Mtaalamu kutoka Chuo cha diplomasia nchini Tanzania anafafanua kuwa suala la uraia pacha linamnufaisha zaidi mtu kuliko nchi husika huku akisisitiza juu ya usalama wa taifa.
“Ni swala linalomnufaisha zaidi mtu anayepewa uraia kuliko nchi husika, na ni ngumu sana kupima uzalendo wa mtu anayepewa uraia pacha hivyo kwa nchi si salama. Na mara nyingine inakuwa changamoto kubwa kuzuia hujuma ambazo mpewa uraia anaweza kufanya kwa nchi mojawapo” anasisitiza mwanadiplomasia huyo.
Kwa kipindi kirefu sasa Tanzania imesimamia msimamo wake wa kutoruhusu uraia pacha kupitia kifungu cha sheria ya Uraia Sura ya 357 Rejeo la 2002, kinacho sema ‘wote walioukana uraia wa Tanzania wanapoteza haki ya kuendelea kuwa Watanzania’.
Hata hivyo katika kuhakikisha mchango wa diaspora unaonekana wazi nchini humo Tanzania ilianzisha mfumo wa kidijitali ili kuorodhesha diaspora wote wenye asili ya Tanzania.
Pia kupitia benki kuu ya Tanzania, nchi hiyo imetoa maelekezo kwa taasisi za kifedha kuwaruhusu diaspora kufungua akaunti za benki za fedha za kigeni kwa kutumia vitambulisho mbadala.