Rais wa Jamhhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa nchi hiyo imo katika mustakbali wa kujiimarisha kama kitovu cha utalii wa kimatibabu, kutokana na kuimarika kwa miundo mbinu na taaluma katika sekta ya afya.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika dhifa ya mchana iliyoandaliwa kwa heshima ya madaktari bingwa wa mifupa kutoka jimbo la California Marekani, alisema kuwa serikali yake inawekeza fedha zaidi katika ununuzi wa vifaa vya kisasa na utoaji mafunzo kwa wataalamu.
''Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, tunazo sasa huduma za CT scan katika hospitali za rufaa za mikoa, huduma ya MRI, katika hospitali kuu za rufaa za Kanda.'' Amesema Mama Samia.
Hata hivyo Rais Samia alikiri kuwa kuna uhaba katika urahisishaji wa huduma hizi kutokana na gharama ya juu.
''Kwa bahati mbaya, kutokana na hali ilivyo kiuchumi, uwezo wa nchi wa kuwatayarisha na kuwatuma wataalamu wa huduma hizi uko nyuma ikilinganishwa na mahitaji yake,'' amesema Rais Samia. ''Lakini naamini tutamudu na hatimaye kusuluhisha hili,'' aliongeza.
Rais Samia alisema kuwa serikali inashughulikia utoaji wa huduma ya bima ya afya kwa wote, kama njia mojawepo ya kulitatua tatizo la gharama ya juu ya afya kwa wananchi.
Tanzania imekuwa ikifaidika na huduma ya kambi ya matibabu kutoka kwa madkatari bingwa wa mifupa kutoka Marekani walioibandika jina na ''Samia Love'' ambapo wamekuwa wakiwatibu wagonjwa mbali mbali wa mifupa pamoja na kuwafanyia uchunguzi waliokuwa wakiumwa.
Mbali na huduma kwa raia, madaktari hao pia wamekuwa wakitoa mafunzo maalum kwa madaktari wa Tanzania juu ya tiba na utumiaji wa teknolojia mpya ya kimatibabu.
'Ni kweli kuwa Tanzania inalenga kujiimarisha kama kitovu cha eneo zima la Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na Kusini kama cha utalii wa kimatibabu,'' aliongeza Mama Samia. ''Mafunzo kama haya yataisaidia nchi hii katika lengo lake hilo.''