Rais wa Tanzania Samia Suluhu aliongoza mkutano wa kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi cha Baraza Maalum la Vyama vya Siasa. Picha: Ikulu
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amejiteteta dhidi ya madai ya kuubana upinzani na kuongeza kuwa wapinzani wameruhusiwa kuandaa mikutano ya hadhara lakini ameonya vikali kuwa, ukiukwaji wowote wa kibali hicho utachukuliwa hatua za kisheria.

Badala yake, ametaka mikutano ya hadhara kutumika kufanikisha mawazo na fikra chanya za kuboresha mwelekeo wa nchi na kutimiza ruwaza ya maendeleo.

Akizungumza baada ya kufungua rasmi mkutano wa kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi cha Baraza Maalum la Vyama vya Siasa uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), rais Samia ameongeza kusema kuwa ameruhusu uhuru wa maoni, lakini sio uhuru wa kutukana.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu aliongoza mkutano wa kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi cha Baraza Maalum la Vyama vya Siasa. Picha: Ikulu

"Mikutano ya hadhara imeruhusiwa, watu wanakwenda, tunayasikia yanayosemwa huko. Tumeruhusu mikutano ya hadhara tukiwa na nia vyama vya kisiasa vizungumze, wananchi wasikie sera zao, mipango yao, ili vyama vikue na virudishe wale waliowapoteza. Vyama visimame, viwe madhubuti ili tukienda kwenye uchaguzi kila chama kimejijenga vya kutosha na ndio maana ya kutoa fursa ya mkutano wa hadhara," alisema.

Lakini Rais Samia amefafanua kuwa hatua ya serikali kuruhusu mikutano ya hadhara haijatoa fursa ya kutumika vibaya kinyume cha sheria.

"Hatukutoa fursa hii ili watu wakavunje sheria, wakasimame kutukana, wakasimame kukashifu, wakasimame kuchambua dini za watu. Kwa sababu ya kuwa hakuna ya kuzungumzwa, tulianza na katiba, bandari, imeenda, sasa katiba tena, hakuna." rais Samia alimaliza.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wa kisiasa, kidini na wakuu wa serikali ya Tanzania. Picha: Ikulu Tanzania

Kiongozi huyo ametoa wito kwa mirengo ya kisiasa na viongozi wake, kuwekeza ipasavyo kupitia uhuru huo na kufufua vyama vyao vya kisiasa kwa mianjili ya chaguzi zijazo.

"Kajijengeni kwa wananchi, elezeni mumejipanga vipi, ili wananchi warudi, wawaunge tena mkono tukienda kwenye uchaguzi vyama vikasimama. Hilo ndilo la kufanya," Rais alimaliza.

Rais huyo ambaye aliwasili muda mchache mkutanoni baada ya kutua kutoka Kizimkazi, Zanzibar, amesisitiza kuwa mwelekeo wa nchi ni suala muhimu kwa nchi nzima na kuwa hakuna yeyote mwenye uwezo wa kuwalazimisha wengine wafuate nyayo zake.

"Tanzania hii inahitaji uendeshaji wake kwa fikra za kila mtu. Hakuna mtu ajitokeze ajifanye yeye ndio Mtanzania kuliko wengine na kwamba uendelezaji uko mikononi kwake, hakuna, ni yetu wote. Na ili tuendeshe vizuri, tupate mawazo yetu sote. Kundi hili litoe mawazo, kundi lile. Mungu katuumba tutofautiane. Kila mtu ana fikra zake," Samia alisema.

Hakuna mtu aliyepewa waraka au hati kwamba wewe ndiye mmiliki wa Tanzania. Tanzania ni yetu sote. Hata kitoto kinachozaliwa leo, kina haki yake ndani ya Tanzania hii.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Rais Samia pia amegusia uhuru wa maoni lakini ameeleza wazi kuwa kuna tofauti ya uhuru wa maoni na uhuru baada ya maoni iwapo maoni hayo yatakiuka sheria.

"Tulitoa Uhuru wa maoni, maoni mengi sana yanatoka kwa watanzania. vijana, wazee, wataalamu, na wanasheria. Kuna uhuru wa maoni, lakini huu uhuru wa maoni una mipaka yake, sio tu kisheria hata kibinaadam." Rais Samia alisema.

"Uhuru wa kutoa maoni una mipaka yake. Mengine tunayoyashuhudia kwenye mitandao, kwa mtu aliyelelewa vizuri, hawezi kuyasema. Si kisheri tu, hata kibinadam."

Hakuna aliye juu ya sheria

"Hakuna aliye juu ya sheria. Hakuna. Kila anayefanya makosa, sheria itamshika, kama umekiuka sheria, sheria itakushika, kwa hiyo tutambue kuwa Hakuna aliye juu ya sheria. ajenda yetu kubwa kama watanzania ni kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Mambo ambayo tumeyafanya miaka yote na sasa tunachofanya ni hicho hicho."

Rais wa Tanzania Samia Suluhu aliongoza mkutano wa kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi cha Baraza Maalum la Vyama vya Siasa. Picha: Ikulu

Tutatofautiana maoni, iutakubalika, sasa katika tofauti hizo, tusiende kutengeneza majambo ambayo yanakwenda kuiweka nchi yetu pahali pasipo pa kukaa nchi yetu. Nchi yetu mungu katuumba na neema, mungu katupa baraka, mungu katuumba vyema, mungu kawaumba waanzania na roho rahimu. Mungu kaiumba Tanzania na sifa pekee yayke.

Tangu kuingia madarakani mwaka 2021, rais Samia amefanya jithada mbalimbali za kukutana na viongozi wengine wa kisiasa kutoka kambi ya upinzani. Pamoja na hayo pia, serikali yake imesaini madhiriano na upinzani yanayotaka kufanyika kwa siasa yenye staha bila kutukanana.

TRT Afrika