Jeshi la Polisi nchini Tanzania, siku ya Jumapili lilitangaza kuzuia maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na vijana kutoka Chama Kikuu cha Upinzani, Chadema wakiwatuhumu kupanga kufanya vurugu.
Siku ya Jumamosi, vijana wa Chadema walitangaza kuwa vijana takribani 10,000 walikuwa wamepanga kukutana jijini Mbeya, kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Vijana Duniani, chini ya kauli mbiu 'Chukua jukumu kwa maisha yako ya baadaye'.
Hata hivyo, Kamishna wa Jeshi la Polisi la nchi hiyo anayehusika na operesheni na mafunzo, Awadh Haji, alisema kuwa vijana hao walilenga kutumia mwamvuli wa maandamano hayo "kusababisha vurugu na vitendo vingine vya kihalifu."
'Marufuku ya mikusanyiko'
"Polisi wameamua kupiga marufuku aina yoyote ya mikusanyiko ya ndani na ya hadhara au maandamano kwa kisingizio cha kuadhimisha siku ya vijana," alisema Kamishna huyo.
Viongozi wa Chadema wamelaani uamuzi huo, na kumtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati, akiwatuhumu kuzuia misafara ya chama kuelekea Mbeya na baadhi ya watu kukamatwa.
Tangu aingie madarakani mwaka 2021, kufuatia kifo cha ghafla cha mtangulizi wake John Pombe Magufuli, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mfuasi wa mageuzi ya kisera, ikiwemo kulegeza baadhi ya sheria na kanuni kali dhidi ya vyombo vya habari na vyama vya upinzani.
Mnamo Januari 2023, aliondoa marufuku dhidi ya mikutano ya upinzani iliyowekwa mnamo 2016 na Magufuli.
'Mbinu za ajabu'
"Rais Samia usilete mambo ya ajabu ya Magufuli, Siku ya Vijana Duniani inaadhimishwa duniani. Kwanini polisi wako wanawazuia vijana wa Chadema barabarani na kuwakamata?" alihoji Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu kwenye mtandao wa X.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa maandamano hayo ya Jumatatu yataendelea kama yalivyopangwa. "Huu sio wakati wa kukaa kimya, kuogopa, au kuzungumza tu. Ni wakati wa kusimama na kuhesabiwa. Tupaze sauti zetu kwa nguvu zetu zote!"
Lissu, mgombea wa zamani wa Urais alirejea nchini humo baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhitimisha miaka mitano aliyokaa uhamishoni kufuatia jaribio la kutaka kumuua mwaka 2017.
Machi 2022, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliachiliwa huru miezi saba baada ya kukamatwa saa chache kabla ya chama hicho kufanya kongamano la kudai marekebisho ya katiba.
'Vitendo haramu'
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika naye alimtaka Rais Samia Suluhu Hassan na Jeshi la Polisi la nchi hiyo kuacha vitendo visivyo halali.
"Zuia zuia na kamata kamata hii ni kinyume na haki na ni dharau kwa 4R mnazojinasibu nazo," aliandika Mnyika kwenye ukurasa wa X.
Tanzania inatarajiwa kufanya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge mwishoni mwa mwaka 2025.