Tanzania na Jamhuri ya Korea zimetia saini tamko la pamoja kuhusu Uanzishwaji wa Majadiliano juu ya Mkataba wa Ushirikiano Kiuchumi./Picha:Ikulu-Tanzania 

Tanzania na Jamhuri ya Korea zimekubaliana kuanzisha Mkataba wa Ushirikiano wa Uchumi (EPA).

Mkataba huo utaiwezesha Tanzania kupokea mkopo kutoka Korea wa kiasi cha Dola za Kimarekani Bilioni 2.5 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia kuanzia 2024 hadi 2028.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu , Zuhura Yunus kutoka Seoul, Jamhuri ya Korea imesema kuwa, fedha hizo ambazo ni kwa ajili ya miradi ya miundombinu ya maendeleo, zinatolewa chini ya Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi wa Serikali ya Korea (EDCF).

"Ili kufungua milango zaidi ya ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi, Tanzania na Korea zimesaini pia mkataba wa EPA utakaowezesha kuufanya uhusiano kuwa wa kimkakati hususan katika Nyanja za Biashara, Uwekezaji, Viwanda, Usafirishaji na kadhalika," imesema taarifa hiyo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 3 tu barani Afrika ambazo zitafanya majadiliano hayo yatakayozaa Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Korea. Nchi zingine ni Morocco na Kenya./Picha: Ikulu-Tanzania

Tanzania ni miongoni mwa nchi 3 tu barani Afrika ambazo zitafanya majadiliano hayo yatakayozaa Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Korea. Nchi zingine ni Morocco na Kenya.

Hati za Makubaliano zilizotiwa saini kati ya nchi hizo mbili ni pamoja na Ushirikiano katika Uchumi wa Buluu ambapo Tanzania itashirikiana na Korea Kusini katika maeneo ya uvuvi, viwanda vya kuchakata mazao ya bahari, ujenzi wa bandari za uvuvi, teknolojia na tafiti za masuala ya bahari.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara rasmi ya siku mbili 2, na anatarajia kuanza ziara ya kikazi ambapo atahudhuria mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kati ya Korea na Afrika.

TRT Afrika