Rais Samia aliwataka viongozi kutafakari na kuchambua kwa dhati masuala ya rushwa Picha : Ikulu Tanzania

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa Afrika wazungumze kwa sauti moja na kushirikiana katika kuangamiza rushwa na ufisadi kwa jumla barani Afrika.

Mama Samia amesema mojawapo ya vikwazo vikubwa vya maendeleo barani Afrika ni ''pamoja na janga la rushwa ambalo linadhoofisha taasisi mifumo y akitaasisi na kuathiri mipango ya kujikombo akiuchumi.''

''Viongozi wote barani Afrika hawana budi kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya rushwa,'' alisema Rais Samia.

Tahadhari ya hatari ya rushwa na ufisadi

Mama Suluhu alikuwa akihutubia hafla ya maadhimisho ya siku ya kupambana na rushwa duniani na miaka 20 ya mkataba wa umoja wa Afrika wa kuzuia na kupambana na rushwa.

Rais Samia aliwataka viongozi kutafakari na kuchambua kwa dhati masuala ya rushwa ili kubainisha changamoto au vikwazo vya mapambano hayo ili kuvishughulikia.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Transparency International, linalochunguza viwango vya ufisadi duniani, mataifa 155 duniani hayakupiga hatua zozote kupiga vita ufisadi au wengine kuporomoka zaidi katika ngazi y auadilifu.

Transparency International inasema kuwa amani duniani imekuwa ikizorota kwa miaka 15 na ufisadi umekuwa sababu kuu ya hili.

Ripoti hiyo pia ilisema kuwa Ufisadi hudhoofisha uwezo wa serikali wa kulinda watu na kuondoa imani ya umma, na hivyo kuchochea zaidi na kushindwa kudhibiti vitisho kwa usalama.

Mkurugenzi wa shirika la Transparency International alinukuliwa katika ripoti hiyo kusema,''Viongozi wanaweza kupiga vita ufisadi na kuendeleza amani kwa wakati mmoja.''

''Serikali lazima zifungue nafasi ya kujumuisha umma katika kufanya maamuzi - kutoka kwa wanaharakati na wamiliki wa biashara hadi jamii zilizotengwa na vijana. Katika jamii za kidemokrasia, watu wanaweza kupaza sauti zao kusaidia kung'oa rushwa na kudai ulimwengu salama kwa ajili yetu sote.'' aliongeza.

Kwa upande wake Rais wa Tanzania Samia Suluhu amesema serikali yake inaendelea kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU.

TRT Afrika