Mwishoni mwa wiki iliyopita, picha za video zinazomwonesha mwanamke akidhalilishwa kijinsia na kundi la wanaume watano zilisambaa mitandaoni kwa kasi na kuibua hisia tofauti, huku watetezi wa haki za binadamu wakitaka mamlaka husika kuchukua hatua za haraka dhidi ya watuhumiwa.
Katika taarifa yake, Jeshi la Polisi nchini Tanzania kupitia msemaji wake David Misime lilisema kuwa linaendelea na uchunguzi wake licha ya kutothibitisha kukamatwa kwa mtu yeyote. Hata hivyo, jeshi hilo liliuhakikishia umma wa Watanzania kuwa taarifa zaidi itatolewa mara tu mchakato wa kisheria utakapokamilika.
Jeshi la Polisi, pia limewaasa wananchi kutoendelea kusambaza picha hizo, likisisitiza umuhimu wa kumlinda muathirika wa tukio hilo na familia yake.
Aidha, Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Hamad Yussuf Masauni alikiri kukamatwa kwa baadhi ya watuhumiwa, japo hakutoa taarifa zaidi.
Tukio hilo lilionekana kwa mara ya kwanza kupitia akaunti ya Boniface Jacob, Meya wa zamani wa Ubungo jijini Dar es Salaam siku ya Agosti 4, kupitia chapisho lake kwenye ukurasa wake wa X. Kulingana na mwanasiasa huyo, watuhuhimiwa wa tukio hilo wanahusishwa na Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ).
Kwa upande wao, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kililaani tukio hilo, likiliita kama uvunjaji mkubwa sheria.
Msichana Initiative, shirika lililojkita katika kutetea haki za wasichana nchini Tanzania, pia lilitoa wito wa hatua za dharura dhidi ya waliohusika na "vitendo vya kikatili." Walikosoa kuendelea kusambazwa kwa video hiyo mtandaoni, wakisema kwamba inaongeza aibu kwa mwathiriwa.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), kilimsihi Rais Samia Suluhu Hassan kulaani hadharani shambulio hilo, likionya kuwa kushindwa kushughulikia masuala kama haya kunaweza kusababisha ongezeko la matukio hayo chini ya kivuli cha matumizi mabaya ya mamlaka.