Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Tanzania, kupitia idara yake ya uhamiaji imesisitiza kuwa haijasitisha utoaji wa Visa kwa wageni kwenye vituo vya kuingilia na kutoka nchini humo.
Hata hivyo Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania, imeshauri wageni wanaopenda kutembelea nchi hiyo kwa madhumuni mbalimbali, kufanya maombi ya vibali hivyo kwa njia ya mtandao, ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
“Kuomba Visa kabla ya kuingia nchini, mgeni anakuwa na uhakika wa safari yake na hupunguza msongamano na muda wa kuhudumiwa wakati wa kuingia nchini Tanzania,” ilisomeka taarifa hiyo iliyotolewa na Msemaji wa Idara hiyo, Paul Mselle.
Kwa upande mwingine, Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania imewahakikishia wasafiri wanaolekea nchini humo kuwa itaendelea kutoa huduma bora zenye kukidhi viwango vya Kitaifa na Kimataifa.