Wataalamu wa afya Tanzania wametoa tangazo kuondoa hofu ya kutokea mlipuko mpya wa ugonjwa wa Uviko 19, baada ya fununu kusambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu ongezeko la maambukizi.
Waziri wa afya nchini humo Ummy Mwalimu amesema kuwa japo kuna visa vilivyoripotiwa, hakuna vifo vyovyote vilivyotokana na maambukizi hayo.
‘‘Watu 6 kati ya 288 walithibitishwa kuwa na corona. Hii ikiwa ni pungufu ikilinganishwa na wiki ya tarehe 29/04/23 hadi 05/05/23. Hakuna kifo kilicho thibitishwa kusababishwa na UVIKO-19’’
Daktari Elisha Osati, ameambia TRT Afrika kuwa visa vinavyoripotiwa sasa vinatokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
‘‘Tumeingia msimu wa mvua, kwa hiyo, ni jambo la kawaida kuona maambukizi ya magonjwa ya kupumua kuongezeka.’’ Amesema daktari Osati, ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya kifua na magonjwa ya ndani.
Habari zimesambaa katika mitandao ya kijamii baada ya vifo vya baadhi ya watu mashuhuri Tanzania, ambapo wengine wamehusishwa na maambukizi ya Uviko-19.
Daktari Oseta amesema kuwa hakuna ushahidi wowote unaohusisha vifo hivyo na Uviko19.
Daktari Oseta ameongeza, ‘‘ Wakati wa mvua, mara nyingi vimelea na virusi husambazwa kwa urahisi na hubadili maumbile na kuwa sugu. Hili ni jambo la kawaida, ndio maana utaona watu wengi zaidi wanakuja na dalili za homa na mafua’’
Kwa upande wake Waziri wa Afya wa Tanzania Ummy Mwalimu amewashauri watu kuendelea kutii kanuni za afya ili kuepuka maambukizi ya aina yoyote.
COVID 19 sio janga la afya
Mapema mwezi huu, 5 Mei 2023, shirika la afya duniani (WHO) lilitangaza kumalizika kwa Uviko-19 kama janga la kiafya kimataifa.
Hii ni baada ya kupungua au kukosa visa vipya vya maambukizi ya ugonjwa huo.
Takwimu kutoka kwa kituo cha kudhibiti magonjwa barani Afrika , CDC, zinaonesha kuwa, Kufikia 10 Mei, 2023, jumla ya maambukizi milioni 12,295,935 yalikuwa yameripotiwa kutoka kwa mataifa 55 ya Afrika, tangu kuzuka kwa janga hilo.
Pia Afrika imeripoti vifo 257,045 ikiwa ni 4 % ya vifo vyote vilivyoripotiwa diuniani kutokana na ugonjwa huo.
Daktari Elisha Osati, ambaye ni mchambuzi pia wa masuala ya afya, anasema kuwa licha ya tangazo la WHO kuwa Uviko-19 sio janga la kiafya, haina maana kuwa Uviko imeangamizwa kabisa.
‘‘Kwa kuwa WHO imesema Uviko-19 sio janga, usifikirie imekwisha. Ndio maana utaona visa vichache hapa na pale vinaripotiwa.’’ Daktari Osati amesema.
‘’Ni lazima tuendelee na kanuni muhimu kama kuendeleza utoaji chanjo, kuepuka mikusanyiko mi kubwa na mengine,’’ aliongeza.
Hatua za kuchukua kuzuia maambukizi ya Uviko-19.
- Vaa Barakoa ukiwa karibu na umati
- Funika mdomo wako kwa kitambaa unapokohoa au kupiga chafya
- Epuka mikusanyiko isiyo ya dharura
- Safisha mikono yako kwa sabuni na maji ya kutiririka kila mara
- Tumia dawa ya homa au kikohozi punde tu unapoanza kupata dalili hizo
- Nenda ukapimwe ili ujue kwa uhakika iwapo umeambukizwa na Uviko-19.
- Kapate chanjo ya Uviko-19. Kumbuka chanjo yoyote inafaa.
Takwimu za hivi punde
Tangu mwanzoni mwa Mei 2023, vifo 11 vimeripotiwa kutokana na Uviko Afrika, huku maambukizi 1,441 mapya yakiripotiwa ambayo ni kupungua kwa 11%, maambukizi ikilinganishwa na wiki iliyotangulia.
Kituo cha Africa CDC kinasema kuwa nusu ya maambukizi hayo yametokea kaskazini mwa Afrika, huku 1% ikiwa Mashariki mwa Afrika.
Kufikia sasa zaidi ya chanjo bilioni 1.1 zimetolewa Afrika, huku zaidi ya watu milioni 431 wakiwa wamepata chanjo kamili.
Eritrea ndilo taifa la pekee Afrika ambalo halijaanza kutoa chanjo dhidi ya Uviko-19 .