Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania (EWURA), imetangaza bei mpya za mafuta ya petroli zitakazotumika kuanzia, Agosti 7, 2024.
Watumiaji wa nishati ya Petroli katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam, sasa watalazimika kulipia Dola 1.20 (Shilingi za Kitanzania 3,231)kwa lita ya Petroli na Dola 1.16(Shilingi za Kitanzania 3,131) kwa Dizeli, kwa mwezi Agosti.
"Gharama za bidhaa za mafuta zinajumuisha bei ya mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji ambazo ni gharama za usafirishaji, bima na gharama na faida za mleta mafuta kabla ya kodi, tozo na gharama nyingine za hapa nchini," imesema EWURA katika taarifa yake kwa umma.
Kwa mujibu wa mdhibiti huyo, gharama ya mafuta yanayopokelewa na gharama za uagizaji zinalipiwa kwa kutumia fedha za kigeni ikiwemo Dola ya Marekani na sarafu za nchi nyingine.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko, kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166.
Pia, imevitaka vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.