Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania (EWURA), imetangaza bei mpya za mafuta ya petroli zitakazotumika kuanzia, tarehe 3 Aprili 2024.
Kulingana na taarifa iliyowekwa kwenye tovuti ya Mamlaka hiyo, mabadiliko hayo ya bei yamechangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo kuongezeka kwa bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia kwa wastani wa asilimia 3.94 kwa mafuta ya petroli.
Kufuatia mabadiliko hayo, watumiaji wa nishati ya petroli katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam, sasa watalazimika kulipia Shilingi za Kitanzania 3,257 (Dola 1.26) kwa lita, badala ya 3,163 (Dola 1.23) , kwa mwezi Machi.
Mabadiliko katika soko la kimataifa, pia yameathiri bei ya dizeli kwa rejareja, ambayo kwa sasa, nishati hiyo itanunulika kwa Shilingi za Kitanzania 3,210 ( Dola1.24) kutoka 3,126(1.21).
Kwa mujibu wa EWURA, mabadiliko hayo yamechangiwa na kuongezeka kwa kiwango cha kubadilishia fedha za kigeni kwa asilimia 3.19 kutokana na ongezeko la matumizi ya sarafu ya EURO kulipia mafuta yaliyoagizwa.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko, huku EWURA ikiendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta, kulingana na Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166.
"Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika", taarifa hiyo iliongeza.