Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika, ametoa onyo kali kwa wanachama, wagombea na mawakala wa wagombea kuhusu ukiukwaji wa michakato ya uchaguzi wa ndani wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.
Akizungumza jijini Dar es Salaam siku ya Januari 7, Mnyika amesema ni vyema kwa makundi hayo kufuata kanuni na taratibu za uchaguzi zilizowekwa kuanzia mwaka 2012, ili kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa wa huru na wa haki.
Kulingana na Mnyika, kanuni na miongozi hiyo inalenga kuondoa mianya yote ya rushwa wakati wa kampeni na uchaguzi mwenyewe.
Mnyika alisisitiza kuwa atakayebaini ukiukwaji wa miongozi hiyo, atoe taarifa kwenye ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho pamoja na mamlaka zingine, ili hatua kali za kisheria zichukuliwe.
“Ningependa kukumbushia kuwa mtu yeyeto atakayebaini ukiukwaji wa kanuni hizo zilizowekwa, atoe taarifa mapema ili hatua stahiki zichukuliwe,” alisema Mnyika.
Katibu Mkuu huyo wa CHADEMA pia ameonya kuingiza udini, ukabila na ukanda wakati wa kampeni na mchakato mzima wa uchaguzi.
Chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania kiko katika mchakato wa uchaguzi wa ndani, huku wajumbe wake wakichagua viongozi wao kuanzia ngazi ya kanda hadi ya kitaifa.