Kuoshwa miguu kwa waumini ni moja ya ishara zinazotawala siku ya Alhamisi Kuu./Picha: Wengine

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Mabilioni ya Wakristo ulimwenguni wanaanza juma kuu leo kupitia siku ya Alhamisi Kuu.

Siku hii ni sehemu ya maadhimisho ya fumbo kuu la Pasaka, ambalo hutawaliwa na adhimisho la Karamu ya Mwisho, kabla ya kukamatwa, kuteswa, kusulubiwa na kufa msalabani, zaidi ya miaka 2000 iliyopita.

Wakristo, hasa wa dhehebu la Katoliki wanaamini kuwa hii ndio siku aliposhiriki karamu ya mwisho na wafuasi wake, kabla ya kuingia katika mateso yake, baada ya kuuzwa na kusalitiwa na Yuda Iskariote, ambaye naye alikuwa sehemu ya karamu kabla ya kumsaliti Yesu kwa vipande 30 vya fedha.

Hii ndio siku ambayo Wakristo Wakatoliki wanaamini kuwa Yesu Kristo aliweka Amri Kuu ya matendo, kutokana na fumbo hilo la kuaanda karamu iliyoambatana na kitendo cha kuwaosha miguu kama alivyosema, "Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo."

Pamoja na mambo mengine yanayofanyika siku hii, tukio la kuoshwa miguu, ambalo hufanywa na Padri au Askofu ndilo lililojizoelea umaarufu zaidi.

Ukiacha kitendo cha kuoshwa miguu, hii ndio siku ambayo Yesu Kristo aliweka fumbo la Ekaristi Takatifu, fumbo lenye maana kubwa sana katika historia ya Kanisa Katoliki Duniani./Picha: Wengine

Kwa mujibu wa historia, Wayahudi walipendelea kuvaa malapa au kandambili zenye kamba zilizofungwa kwenye kisigino.

Kutokana na Israeli kuwa nchi yenye joto kali, mara nyingi miguu ilipata joto na kutoka majasho yaliyosababisha miguu yao kutoa harafu.

Pia, kutokana na Israel kuwa nchi yenye jangwa kwa sehemu kubwa, ilifanya miguu yao iwe na vumbi hasa wakati wa kutembea.

Hivyo ikiwa Myahudi atapata mgeni nyumbani kwake, tendo la kwanza ni kumuosha miguu kabla ya mgeni kuingia ndani.

Kwani mgeni alipaswa kuvaa malapa ili kuosha au kuoshwa miguu yake. Tendo hili lilikuwa la ukarimu kwa mgeni, maana lilikuwa na malengo makubwa mawili ambayo kwanza ni kipooza miguu kwa mgeni, ambayo kwa sababu ya kutembea imechemka sana kutokana na joto kali na kuisafisha miguu iwe safi, kutokana na kupata vumbi.

Ukiacha kitendo cha kuoshwa miguu, hii ndio siku ambayo Yesu Kristo aliweka fumbo la Ekaristi Takatifu, fumbo lenye maana kubwa sana katika historia ya Kanisa Katoliki Duniani.

Neno Ekaristi asili yake ni lugha ya Kigiriki Eucharistein likimaanisha shukrani. Ekaristi Takatifu ni sadaka ya shukrani kwa Mungu Baba kwa njia ya Yesu Kristo. Ni ukumbusho wa mateso, kifo na ufufuko wake.

Baada ya Alhamisi, Wakristo Wakatoliki huadhimisha siku ya Ijumaa Kuu, wakikumbuka siku ya kuteswa kwa Bwana wao Yesu Kristo.

Kulingana na Amri za Kanisa hilo, waumini wa dhehebu hilo hawaruhisiwi kula nyama siku hiyo, ikiwa ni ishara ya maombolezo na tafakari ya kina ya mateso ya Yesu.

Siku ya Ijumaa Kuu Kanisa haliadhimishi Sadaka ya Misa Takatifu kwa sababu ni siku ambapo wakristo huamini kuwa Yesu mwenyewe alijitoa Sadaka msalabani.

Hali kadhalika, siku ya Jumamosi Kuu Kanisa haliadhimishi Sadaka ya Misa Takatifu, liko kimya likiyawaza mateso na kifo cha Yesu huku madhabahu zikiwa tupu, mpaka zitakapoanza sherehe za Pasaka baada ya Kesha Takatifu au Kesha la ufufuko.

TRT Afrika