Rais Ruto amuunga mkono Papa Francis kuitisha kukomeshwa ghasia Sudan na DRC

Rais Ruto amuunga mkono Papa Francis kuitisha kukomeshwa ghasia Sudan na DRC

Viongozi hao walizungumza katika mkutano wa viongozi wa nchi 7 tajiri duniani uliofanyika Italia
Rais William Ruto amesema AU inajifanyia mabadiliko ili kujiweka kama wakala wa amani katika bara hilo na duniani. Picha / Ikulu Kenya.

Rais wa Kenya WIlliam Ruto amesema kuwa nchi yake inaunga mkono wito wa Papa Francis, wa kusitishwa mapigano na kupatikana amani ya kudumu nchini DRC na Sudan.

Rais Ruto aliyasema haya baada ya kikao cha faragha na kiongozi huyo wa kanisa Katoliki, wakati wa mkutano wa nchi 7 tajiri duniani (G7) uliofanyika mjini Apulia, Italia.

''Tuna imani kwamba makundi yanayopigana yatakubali kusitisha mapigano na kutoa nafasi ya amani,'' alisema Rais Ruto katika taarifa fupi katika mtandao wa X.

Katika fursa nadra ya kuhutubia mkutano huo wa G7, Rais Ruto alisisitiza haja ya jamii ya kimataifa kuwajibikia suala la upatanishi kuondoa migogoro ya duniani.

''Ninatoa wito kwa viongozi wa dunia kuhamasishwa kuchukua hatua kabambe ya pamoja ili kukabiliana na matatizo ya kimataifa,'' alisema Rais Ruto.

AU - Wakala wa amani

Rais Ruto pia aliweka wazi mipango wa mataifa ya Afrika ya kufanya marekebisho ya kimkakati na dhamira ili kuweza kukabiliana na majanga, ikiwemo migogoro ya ndani.

''Afrika imedhamiria kutekeleza sehemu yake kikamilifu, na ndiyo maana AU imewekewa mageuzi makubwa ya kimkakati ili kuwa wakala muhimu, unaotambuliwa na kushughulikiwa na jumuiya ya kimataifa ili kushughulikia changamoto zetu za pamoja na kukuza ustawi wetu wa pamoja,'' alisema Rais Ruto.

Rais Ruto alikuwa miongoni mwa viongozi waliohutubi amkutano wa G7 ambao kawaida ni wa viongozi wa nchi tajiri duniani. / Picha : Ikulu Kenya. 

Ajenda kuu ya mkutano huo ulikuwa uhamiaji, akili mnemba na usalama wa kiuchumi, viongozi wa G7 walisisitiza azma yao ya kukabiliana na changamoto za kimataifa "katika wakati muhimu katika historia."

Hata hivyo msaada wa kifedha kwa Ukraine, vita vya Gaza, mabadiliko ya hali ya hewa, Iran, hali ya Bahari ya Shamu, usawa wa kijinsia na sera ya viwanda na usalama wa kiuchumi wa China vilionekana kutawala mkutano.

Mgawanyiko uliibuka wakati wa mkutano huo, hata hivyo, haswa juu ya kukosekana kwa marejeleo ya uavyaji mimba katika tamko la mwisho la mkutano huo.

Lakini alipoulizwa na waandishi iwapo kuna muafaka juu ya migogoro mikubwa duniani, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikemea kuwa hilo halikuwa sababu yamkutanu huo.

"Lengo la G7 ni kuunda muunganiko na kuweza kuondoa kutokuelewana. Sio mahali ambapo unaamua hatua za dharura au kudhibiti mambo," alisema Macron.

Mbali na mataifa ya G7 ya Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani, wenyeji wa Italia pia waliwaalika viongozi kadhaa wa Afrika - Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune, Rais wa Kenya William Ruto na Rais wa Tunisia Kais Saied.

Lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu yalikashifu kile walichokisema ni ukosefu wa ari ya kuunga mkono nchi zinazoendelea.

TRT Afrika