Mwalimu Nyerere akiteta jambo na Mtakatifu Yohane Paulo wa II./Picha: Wengine

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Hata baada ya kifo chake, miaka 25 baadaye, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anabakia kuwa mwanasiasa pekee ulimwenguni kupata hadhi ya Mtumishi wa Mungu, ambayo ni hatua mojawapo kati ya tatu ya kufikia kuitwa Mtakatifu ndani ya Kanisa Katoliki, lenye makao makuu yake huko Roma.

Kulingana na Kanisa Katoliki duniani, ili mtu aweze kutangazwa kuwa Mtakatifu, basi ni lazima apitie hatua za Utumishi wa Mungu na Uenyeheri.

Licha ya kutangazwa kuwa Mtumishi wa Mungu, mchakato wa Mwalimu Nyerere kufikia hatua ya kuitwa Mtakatifu bado unaendelea ndani ya Kanisa Katoliki, huku ukiendelea kupewa chagizo na Baraza Kuu la Maaskofu nchini Tanzania (TEC), na Rais Yoweri Museveni wa Uganda.

Mchakato wa Utakatifu

Mchakato wa kumtangaza Julius Kambarage Nyerere kama Mtumishi wa Mungu, ulianzishwa na Askofu Justin Samba, na kuendelezwa na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma kabla ya kutua rasmi kwenye Jimbo Kuu la Dar es Salaam mwaka 2019, ambapo ndipo yalipo makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Tofauti na inavyofahamika na wengi, mtu yeyote ndani ya Kanisa Katoliki anaweza kupitia hatua hii, sio lazima awe mtawa, kama ilivyo kwa Mwalimu Nyerere.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni akisalimiana na mjane wa Mwalimu Nyerere, Mama Maria Nyerere kwenye moja ya hija za Namugongo nchini Uganda./Picha: Wengine

Hata hivyo, Kanisa Katoliki duniani haliwafanyi watu kuwa Watakatifu, bali linatangaza kuwa mmoja amefikia utakatifu baada ya kuwa na viashiria vingi vinavyodhihirisha hilo.

Ni kwa sababu hii basi, TEC kupitia tangazo lake la Julai 25, 2023, limeijulisha Jumuiya ya Kanisa kuhusu jambo hilo, na kuwaalika waamini wote kuwasiliana na Baraza hilo moja kwa moja au kwa kutuma kwenye Mahakama ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam inayoshughulikia mchakato huo.

“Kwa tangazo hili, tunaelekeza kwamba, yeyote ambaye ana maandiko hayo ayatume kwa umaini kwa Mahakama hiyo iliyotajwa, nyaraka zozote zilizoandikwa na Mtumishi wa Mungu ambazo bado hazijakabidhiwa kwa Mratibu kwa mchakato,” ilisomeka sehemu ya tangazo hilo la TEC.

Tofauti na inavyofahamika na wengi, mtu yeyote ndani ya Kanisa Katoliki anaweza kupitia hatua hii, sio lazima awe mtawa, kama ilivyo kwa Mwalimu Nyerere./Picha: Adarsh Nayar

Museveni apigia chapuo mchakato huo

Pamoja na tangazo la TEC kuitaka Jumuiya ya kanisa kupeleka maoni yao na ushahidi wao kuhusu maisha ya Mwalimu Nyerere, Rais wa Uganda Yoweri Museveni naye ameendelea kupigia chapuo mchakato huo.

Mara kwa mara, kiongozi huyo wa Uganda ametaka kuharakishwa kwa mchakato wa kumtangaza Mwalimu Nyerere kama Mtakatifu, akiamini kuwa maisha yake na uongozi wake unasadifu sifa hiyo.

Nawapongeza ndugu zetu kutoka Tanzania mkiongozwa na Mama Maria Nyerere kuja kufanya hija hapa Namugongo na pia kuja kumuombea Mwalimu Nyerere ili atangazwe kuwa Mtakatifu,” alisema Rais Museveni wakati wa hija ya Namugongo, mwezi Juni 2024.

Hata katika mazungumzo yake binafsi na Mama Maria Nyerere, Rais Museveni hakusita kulirudia jambo hilo, huku akisisitiza:

“Nafurahia sana jambo hili la kumtangaza Mwalimu Nyerere kuwa Mtakatifu.”

Mwalimu akiwa na viongozi wa Kanisa Katoliki kwenye Kanisa la Mt Yosefu, jijini Dar es Salaam, Tanzania./Picha: Adarsh Nayar

Maisha ya uadilifu

Katika risala yake aliyoitoa mwezi Aprili, 2022, Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Jaji Joseph Warioba alimuelezea Mwalimu Nyerere kama mtu muadilifu.

Kulingana na Jaji Mkuu huyo mstaafu, Mwalimu Nyerere alikuwa mtu muadilifu, muaminifu na mwenye nidhamu kwa nchi yake na ndio maana aliichukia rushwa.

“Wapo hapa ambao tulifanya naye kazi katika lile baraza la mawaziri na alitaka kila waziri awe amejiandaa kikamilifu siku ya kikao cha baraza na yeyote atakayechelewa, basi atafungiwa kwa nje,” alisema Warioba.

Mwalimu Nyerere aliichukia rushwa./Picha: Wengine

Baba huyo wa Taifa la Tanzania anaendelea kukumbukwa kama mtu mwenye huruma aliyeishi maisha ya kawaida akijali zaidi maslahi ya taifa lake.

Mwalimu Nyerere atakumbukwa sana kwa maisha yake ya kujitolea hasa alipoamua kuwa mstari wa mbele kupigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika zikiwemo Angola, Msumbiji, Namibia, Zimbabwe na Afrika Kusini.

TRT Afrika